Muda wa mashabiki wa Chelsea kusema “kwaheri” kwa mshambuliaji wao matata na msumbufu, Mbelgiji Eden Hazard umewadia.
Mshambuliaji huyo mwenye miaka 28, huku akiwa amesaliwa na mkataba wa mwaka mmoja na miezi kadhaa na klabu yake ya Chelsea, Hazard amefunguka kuwa, muda wowote atafanya maamuzi magumu katika kujenga mustakabali mzuri wa maisha yake katika soka na kuepuka majuto katika siku za mwisho za kusakata kabumbu.
Akizungumza na kituo kimoja nchini Uingereza Hazard amesema kuwa, kuanzia kitambo amekuwa na ndoto ya kuichezea klabu ya Real Madrid na anaamini ndoto yake itatimia siku moja.
“Mimi, unajua mimi nimekuwa nikiipenda Real Madrid tangu kitambo”.
Wengi wanaamini kuwa Hazard alikuwa chaguo la kocha Mfaransa Zinedine Zidane, na kwa sasa hana nafasi kubwa kwa klabu hiyo ya Hispania lakini kwa upande wake, Hazard ameyakataa maneno hayo na kusema kuwa yeye anaipenda Madrid kabla na hata baada ya Zidane kuondoka.
Akielezea juu ya mazungumzo na klabu yake juu ya kuongeza mkataba mpya, Hazard amesema kuwa, baada ya kombe la dunia klabu ilianzisha mazungumzo juu ya kuongeza mkataba mpya, lakini kwa sasa zoezi hilo limesitishwa lakini yeye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho
“ Kama nilivyosema nitamaliza mwaka huu nikiwa na Chelsea na nitabakiza mwaka mmoja, tutaona nini kitatokea”
Mshambuliaji huyo alisema kuwa kocha mpya wa Chelsea, Maurizio Sarri anaamini kuwa, mfumo wake unaendana na uwepo wake ndio maana Sarri anafanya kila juhudi kuhakikisha Hazard anasalia darajaani. Mkataba wa Hazard na Chelsea unamalizika mwaka 2020.
Hadi sasa, Hazard ameifungia Chelsea goli 7 na kutoa
pasi za mwisho 8 katika mechi 15 za ligi alizocheza msimu huu 2018-19, huu ni wastani mzuri.