Sambaza....

Kocha mpya wa Real Madrid Zinedine Zidane amezima ndoto za mashabiki wengi kumuona Cristiano Ronaldo anarejea kwenye klabu hiyo baada ya hapo jana Zidane kutangazwa kocha mpya ikiwa ni miezi 10 tu toka atangaze kuachia ngazi kwenye klabu hiyo.

Zidane alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Ronaldo kurejea Real Madrid amesema kwa sasa hilo sio la muhimu kwani bado wanamichezo 11 kwenye ligi na pengine wanatakiwa kuweka mkazo katika michezo hiyo kuliko kuwaza kama Ronaldo atarejea Madrid ama laa.

“Hilo sio jambo muhimu kwa leo, tunamichezo 11 mbele yetu, baada ya hapo ndo tutajua, hata hivyo wote tunafahamu namna Cristiano alivyo na mchango na historia kubwa kwenye timu yetu, heshima yake kwenye klabu hii ni moja ya jambo kubwa sana, lakini kwa leo sio sehemu sahihi ya kuzungumzia mambo haya,” Zidane amesema.

Jana baada ya klabu hiyo kumtangaza Zidane kurejea, Cristiano Ronaldo aliweka picha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii za Twitter na Instagram picha ambayo wengi waliitafsiri kama pongezi kwa klabu yake hiyo ya zamani na kuonesha dhahiri hamu ya kurejea Uhispania.

Zidane ambaye aliipa mataji matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Real Madrid kabla ya kuachia ngazi mwaka jana, amerejea na kuchukua mahali pa kocha Santiago Solari ambaye naye alichukua mikoba kwa Julen Lopetegui Argote.

Sambaza....