Zinedine Zidane ametangazwa tena kuwa kocha mkuu wa Real Madrid, ikiwa ni baada ya kutimuliwa kwa kocha aliyekuwepo Santiago Solari ikiwa ni miezi tisa tangu ajiengue kama kocha mkuu.
Solari ambaye alikuwa amerithi mikoba ya Julan Lopetegui na kupewa mkataba wa hadi mwaka 2021, ametimuliwa rasmi leo baada ya kupokea vipigo mfululizo mara tatu, ikiwemo dhidi mahasimu wao Barcelona, nyumbani na ugenini kisha kutolewa na Ajax katika hatua ya 16 bora ligi ya mabingwa Ulaya.
Zidane amepewa mkataba wa kuinoa Los Blancos kwa misimu mitatu hadi mwaka 2022, huku timu hiyo ikiwa nyuma ya Barcelona kwa alama 12 na ikiwa imesaliwa na mechi 11 ili msimu kumalizika.
Kupitia tovuti yao, Madrid waliandika ujumbe wenye kichwa hiki “bodi imeamua kuvunja mkataba na Solari, kama kocha mkuu” Klabu inashukuru mchango wa Solari, kujituma na uaminifu vilionekana ndani ya klabu”
“bodi imekubaliana kumteua Zinedine Zidane kama kocha mpya wa klabu, ataanza majukumu yake katika kumalizia mechi zilizosalia La liga msimu huu na misimu mitatu mbele hadi June 30, 2022”
Zidane ambaye aliondoka akiwa ameacha historia kubwa kwa klabu na kwa bara la Ulaya kwa ujumla baada ya kuchukua mataji matatu mfululizo ya klabu bingwa barani humo.
Ujio wake huenda ukaongeza chachu na hamasa ya ushindi, japo amerudi huku akikosa huduma ya mshambuliaji wake tegemeo Mreno Christiano Ronaldo. Ronaldo ambaye aliondoka sawia na Zidane na kujiunga na Vibibi Vizee vya Turin, Juventus.
Ujio wake pia, unaleta fikra za kuondoka kwa straika matata Gareth Bale. Bale hakuwa na mahusiano mazuri na Zidane katika kipindi chake chote akiwa kama kocha mkuu wa miamba hiyo ya soka barani Ulaya.
Bale hakuwahi kuaminiwa hata pale alipoifungia timu yake mabao muhimu ya kuipeleka fainali na kuwafunga Liverpool. Ujio wa Zidane huenda ukawa na athari kwa Bale endapo tu tofauti zao hazitarekebishwa mapema.
Je Barcelona watakubali Zidane abebe ndoo ya La Liga? Unadhani ujio wake utaziba pengo la Ronaldo? Je atarudia kama aliyoyafanya misimu mitatu iliyopita kwa msimu ujao? Vipi kuhusu mahusiano yake na Bale? Unadhani Marcelo atarudi katika kiwango chake za zamani? Tusubiri muda utazungumza mengi.