Tulishuhudia CECAFA, macho yetu yalipendezwa na vingi vilivyotokea Kenya kwenye michuano ya CECAFA.
Furaha ambayo ilipitiliza kiasi kwamba tulitumia kubeza sehemu moja na kusifia sehemu nyingine bila kutuliza akili zetu kwa umakini.
Zanzibar ilisifiwa sana, Tanzania bara ilizodolewa sana, cha ajabu tulifika sehemu ambayo ilitulazimu kusema Zanzibar wana misingi imara ya soka na kama wakipewa uanachama wa FIFA watafuzu kombe la dunia.
Nilishtuka baada ya kusikia maneno hayo, nafsi yangu iliniambia usiingie kwenye mkumbo huo wa kusifia wakati nikiwa na furaha.
Akili yangu ilitulia nikaamua kuandika makala ambayo niliwaambia Zanzibar maeneo wanayotakiwa kuyapitia ili na mimi niwasifie.
Sikutaka kuwasifia Zanzibar na kuwaweka daraja la juu kwa sababu ya kufika kwao fainali ya kombe la CECAFA.
Michuano ambayo haina ushindani na mvuto ndani na nje ya uwanja, michuano ambayo timu za taifa hupeleka vikosi vya vijana kushiriki michuano hiyo.
Michuano ambayo Zanzibar ilitegemea wachezaji wengi wanaocheza ligi ambayo siyo ya Zanzibar, ndiyo maana nikaona hakuna mipango dhabiti katika soka la Zanzibar.
Mipango ambayo inawezesha kutoa timu yenye ushindani wa hali ya juu na kushindana na timu zilizobora.
Ligi yao imekuwa dhaifu miaka nenda rudi, hata baada ya michuano ya CECAFA mwaka huu kulifanyika michuano ya kombe la mapinduzi ambayo vilabu vya Zanzibar vilifanya vibaya.
Hiki ndicho kilichoonesha hali halisi ƴya ligi ya Zanzibar ilivyo.
Ligi imara siku zote hutoa vilabu ambavyo ni imara, vilabu ambavyo vinaweza vikashindana katika ngazi kubwa na kufanya vizuri.
Kushindwa kwao kufanya vizuri katika michuano ya Zanzibar mbele ya timu tano kutoka nje ya Zanzibar ilikuwa ni kielelezo tosha ƙligi kuu yao ni dhaifu.
Udhaifu ambao unatokana na kuendeshwa vibaya kwa ligi hii, hakuna mipango dhabiti ya kuifanya ƙligi hii iwe imara.
Timu yenye timu zaidi ya 20 lakini haina mdhamini, timu zinashiriki katika mazingira magumu, mazingira ambayo hayatoi motisha kwa wachezaji kupigana kwa nguvu zote.
Viongozi wa ZFA wamekaa maofisini bila kufanyia ufumbuzi wa hili jambo.
Hakuna kitu kipya wanachokiwaza ili kuimarisha ligi hii zaidi ya wao kukaa na kuimarisha migogoro kati yao.
Viongozi wa Unguja na Pemba hawana maelewano mazuri kati yao, kuna migogoro kila uchwao.
Migogoro ambayo inadumaza maendeleo ya mpira Zanzibar, badala ya kufikiria namna sahihi ya kuchochoe kuni za maendeleo wao wanawaza namna gani wataongeza majiko ya kupikia migogoro yao.
Kitu kinachopelekea mpaka baadhi ya timu kugoma kushiriki ligi kuu Zanzibar.
Hakuna anayeshtuka kuhusiana na hiki kitu, kitu pekee kitakachowashtua ni wao kuamka siku moja mifuko yao haina pesa.
Watakuna kichwa kuangalia njia sahihi ya wao kushibisha tumbo lao na kusahau kuwa wapo pale kwa ajili ya kushibisha njaa ya wapenda mpira Zanzibar.
Mwisho wa siku ligi inatosha timu dhaifu, timu ambazo haziwezi kushindana ipasavyo kwenye michuano ya vilabu Afrika.
Ndiyo maana haikuwa ajabu Zesco kuwaadabisha JKU magoli saba (7), na hakuna aliyeshtuka kuhusiana na hiki ƙkipigo.
Tunasubiri timu ya taifa iende kushiriki CECAFA ifike fainali ipokelewe kwa shangwe na kuvishwa taji la ushujaa.
Taji ambalo litaenda sambamba na mbwembwe za kuwapa wachezaji viwanja kila mmoja kisa tu wamefika fainali ya kombe la CECAFA.
Kuna wakati bora kipofu anayeona kuliko mtu asiyekipofu na haoni. Inauma sana viongozi wanaposhindwa kuona njia za misingi ya kukuza mpira.
Hakuna anayeona namna ya kukaa kwenye njia ya maendeleo ya mpira.
Vile viwanja waliopewa wachezaji wa timu ya taifa haikuwa njia sahihi ya kutengeneza mkondo wa maendeleo ya soka Zanzibar.
Nilidhani viwanja vile wangepanga kujenga kituo cha kulelea vipaji ili wanufaike kwa baadaye.
Lakini kutokana na furaha kuwazidi walishindwa kuona mbele, macho yao yakabaki kutazama walipokuwa wamesimama.
Ikawa ngumu kufanya hatua moja ya kwenda mbele, kwa sababu walishindwa kutambua njia ya kupitia kwa sababu ya furaha
Mapinduzi na mashindano ya vilabu Afrika yameshatoa funzo tosha kwa mpira wa Zanzibar, wanatakiwa wakae wamalize migogoro waliyonayo, baada ya hapo waangalie namna sahihi ya kujenga ligi yenye ushindani.
Ligi ambayo itatoa washindani kama ilivyokuwa kwa Malindi waliofika nusu fainali katika mashindano ya vilabu Afrika