Sambaza....

Mnamo mwaka 1974, Zaire (sasa DR Congo) ilikuwa nchi ya tatu ya Afrika kushiriki katika Kombe la Dunia la FIFA lakini walipata kipigo ambacho hawatakisahau.

Takriban miezi mitatu kabla ya Kombe la Dunia, walikuwa wameibuka mabingwa wa AFCON baada ya kuifunga Zambia katika fainali na baada ya kumaliza kufuzu kwa Kombe la Dunia, rais wa wakati huo Mobutu Sese Seko Kuku Ngbendu Wa Za ​​Banga aliwaalika kwenye makazi yake na inasemekana wote aliwanunulia magari na nyumba.

Mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia wa Zaire ulikuwa dhidi ya Scotland ambapo walipoteza kwa mabao 2-0. Baada ya mechi, bonasi zao za mechi ziliripotiwa kuzuiwa na serikali.

Wachezaji hawakufurahishwa na kitendo hicho na walikataa kucheza katika michezo iliyofuata. Lakini baada ya kushawishiwa, walikubali kwa shingo bawani (shingo upande).

Katika mchezo wao wa pili dhidi ya Yugolasvia, walikumbana na kichapo kizito zaidi katika historia ya Kombe la Dunia, kwa kufungwa mabao 9-0.

Kwa mujibu wa beki wa Zaire, Mwepu Ilunga, Rais Mobutu aliwatishia baada ya mechi hiyo na kuwaonya kwamba iwapo watapoteza kwa mabao manne katika mchezo utakaofuata dhidi ya Brazil, hakuna hata mmoja wao ambaye angerejea nyumbani.

Waliishia kufungwa mabao 3-0 na Brazil. Katika mchezo huo, wakati Rivelino wa Brazil akijiandaa kupiga mpira wa adhabu, Mwepu Ilunga wa Zaire aliupiga mpira mbali akitegemea kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kitendo chake cha kupinga maamuzi ya refa, lakini alipata kadi ya njano tu.

Kocha mkuu wa zaire Blagoje Vidinić, ambaye alikuwa kutoka Yugoslavia, hakurejea Zaire baada ya michuano hiyo, aliamua alirejea moja kwa moja nchini mwake Yugoslavia.

Wachezaji wa Zaire inasemekana hawakuwahi kulipwa na serikali na pia serikali iliacha kufadhili timu ya Taifa. Pia, hawakuruhusiwa kuondoka nchini na hii ilizuia matarajio yao ya kuhamia vilabu vya Ulaya, na kupoteza ofa zilizokuja baada ya Kombe la Dunia.

Sambaza....