Kocha mkuu wa timu ya Soka ya Yanga ya Mwinyi Zahera ameweka wazi mikakati yake ya kuongeza wachezaji kupitia dirisha dogo la usajili, hukua akiamini itamsaidia kufikia lengo la kurejesha heshima ya kutwaa ubingwa wa Tanzania bara ambao kwa sasa unashikiliwa na Wekundu Wa Msimbazi Simba SC.
Zahera amesema lengo kuu alilojiwekea kuelekea kipindi cha dirisha dogo la usajili ni kuongeza wachezaji watatu ambao hakua tayari kueleza wanacheza nafasi gani uwanjani, huku akithibitisha kuwaacha wengine watatu ambao huenda wakatolewa kwa mkopo.
“Tupo na mpango wa kuongeza wachezaji watatu, na pia tunapunguza wachezaji kati ya watano hadi sita na pengine Saba, tutaongeza wachezaji mbele kati na nyuma, Kati ya hao wawili watatoka nje, mmoja atatoka hapa nchini, na Siwezi kuleta mchezaji nisiye mjua hivyo lazima mmoja awe kutoka Congo lakini anacheza Gabon” Zahera amesema.
Hata hivyo kocha huyo kutoka Jamhuri Ya Kidemokrasia ya Kongo amesema wanaamini wakati akijipanga kufanya maboresho katika kikosi chake, upande wa timu pinzani hali itakua kama ilivyo kwa Yanga, hivyo hatokua na budi ya kuchanga vyema karata zake kwa kuwasajili wachezaji wenye uwezo ambao utaweza kukisaidia kikosi chake.
Kwa sasa Zahera ameondoka nchini kujiunga na Timu ya Taifa ya DR Congo kama kocha msaidizi kujiandaa na michezo ya kuwania kufuzu kwenye fainali za Mataifa Afrika.