KUELEKEA mchezo wao wa 18 msimu huu katika ligi kuu Tanzania bara msimu huu nahodha wa Yanga SC, Kelvin Yondan ‘Vidic’ amesema watapambana kama timu katika game yao vs Mbeya City FC wiki hii.
Timu hizo mbili zinatarajiwa kukutana katika uwanja wa Sokoine, Mbeya Disemba 28. Yanga wanaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya alama saba dhidi ya Azam FC walio nafasi ya pili katika msimamo.
” Tunafahamu ni mchezo mwingine mgumu lakini kama timu tumedhamilia kushinda na kufikisha pointi 50. ” anasema Kelvin nilipofanya naye mahojiano mafupi Jumatano hii.
” Itapendeza kuwa timu ya kwanza katika historia ya ligi kuu Tanzania bara kufikisha pointi 50 ndani ya michezo 18 tu. City ni wazuri na tutaingia uwanjani tukiamini tunakwenda kupambana na timu ngumu, na tutapambana kutimiza malengo yetu.”
Ushindi katika uwanja wa Sokoine wikend hii utawanya mabingwa hao mara 27 wa kihistotia kufikisha alama 50- itakuwa ni rekodi ya haraka zaidi katika historia kwa timu kufikisha pointi 50 baada ya michezo 18 tu katika ligi kuu Bara.
Katika michezo 17 iliyopita kikosi hicho cha kocha Mcongo, Zahera Mwinyi kimeangusha alama nne tu kati ya pointi 51 walizopaswa. Pointi za kwanza waliangusha katika suluhu-tasa dhidi ya mahasimu wao Simba SC na nyingine mbili walipolazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Ndanda FC katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.