Sambaza....

Timu ya Yanga ya Tanzania imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuwashangaza wenyeji Sports Club Villa kwa kuwachapa mabao 2-1 mabao yaliyofungwa na wachezaji Said Mwamba Kizota na winga machachari Edibily Jonas Lunyamila.

Wakishangiliwa na maelfu ya watazamaji Sports Club Villa walifanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya pili tu ya mchezo lililofungwa na winga wake Akena George.

 

Yanga ambao wengi hawakuipa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa baada ya kuanza vibaya michuano hiyo kwa kuchapwa mabao 3-1 kwenye mchezo wao wa kwanza katika kundi lao ilisawazisha bao hilo dakika ya sita tu kupitia kwa mshambuliaji wake hatari Said Nassor Mwamba Kizota ambaye aliibuka mfungaji bora kwa kufunga jumla ya mabao sita.

Zikiwa zimesalia dakika mbili mpira kuwa mapumziko winga machachari Edibily Jonas Lunyamila aiipatia Yanga bao la pili baada yakupita beki  Paul Hasule ambaye aligeuzwa uchochoro siku hiyo na winga huyo mwenye umbo dogo, Lunyamila alipiga chenga iliyompeleka chini beki huyo wa kimataifa wa Uganda na akiwa umbali wa mita ishirini aliachia shuti kali lililojaa wavuni na kumuacha golikipa  Charles Simbwa akigaagaa.

Baada ya kushindwa kuhimili kasi ya winga huyo Paul Hasule alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Charles Omego ambaye naye alipata shida sana kumthibiti Lunyamila ambaye alinyanyasa anavyotaka na kusababisha hatari nyingi langoni mwa Sports Club villa siku hiyo.

Yanga walifanya mabadiliko kwa kumtoa golikipa Steven Nemes aliyeumia na nafasi yake kuchukuliwa na Riffat Said pia Steven Mussa alimpisha kiungo mtukutu Hamisi Thobias Gaga “gagarino.”

Mpaka mwisho wa mchezo Yanga mbili Sports Club Vilaa moja.

Sambaza....