Klabu ya Soka ya Yanga ipo katika hatua nzuri ya kufuzu kwenda nusu fainali baada ya matokeo ya droo ya Kombe la Shirikisho iliyochezeshwa leo usiku nchini Misri.
Katika droo hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika Yanga imepangiwa na Rivers United ya nchini Nigeria na hivyo kukwepa kukutana na vigogo wengine Pyramids Fc ya Misri na USM Algier ya Algeria.
Michezo mingine ya robo fainali itakua ni kati ya Pyramids dhidi ya Marumo Gallants, US Monastir dhidi ya Asec Mimosa na USM Algier dhidi ya AS FAR.
Endapo Yanga itafuzu kwenda nusu fainali itakutana na mshindi kati ya Pyramids au Marumo Gallants ya Afrika Kusini. Michezo ya robo fainali hatua ya kwanza itapigwa kati ya April 21 na 23 na marudiano itakua ni kati ya April 28 na 30 mwaka huu.
Baada ya droo hiyo Rais wa klabu ya Yanga Injinia Hersi Said amesema sasa ni wakati sahihi kwa wao kulipa kisasi kwani msimu uliopita waliwatoa katika hatua za awali.
Hersi Said “Kwetu sisi hii droo ni nzuri zaidi kwa Wanayanga walikua wanatamani tukutane na Rivers zaidi kuliko hizo timu nyingine. Kwetu sisi sasa hiki ni kisasi kama ambavyo tulivyokua na slogan ya kisasi na Monastir sasa tunakihamishia kwa Rivers Nigeria.”
Kwa upande wa Wekundu wa Msimbazi Simba wao watakua na kibarua kigumu mbele ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Wydad Casablanca ya nchini Morocco.
Michezo mingine ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa itakua ni kati ya Al Ahly dhidi ya Raja Casablanca, CR Belouzdaid dhidi ya Mamelody Sundowns na JS Kabyele watakutana na Esperence de Tunis.
Endapo Simba itafuzu na kwenda nusu fainali watakutana na mshindi wa mchezo wa robo fainali ya tatu katika mchezo kati ya CR Belouzdaid au Mamelody Sundowns “The Brazilians”
Michezo ya robo fainali ya msimu huu itaanza kutimua vumbi kati ya tarehe 21 na 22 ya mwezi Aprili na marudiano ni tarehe 28 na 29 ya April pia.
Pia Shirikisho la soka Barani Afrika CAF limethibitisha michezo ya fainali kwa mashindano yote hiyo itafanyika katika mfumo wa nyumbani na ugenini kama ambavyo awali ilikua ikifanyika tofauti na mwaka jana pekee ambapo mchezo wa fainali ulikua mmoja tu.