Waswahili hawana tabia ya kusifia hadharani mambo mazuri hata kama wamependezwa nayo, huu ni ugonjwa tulionao na tunaishi nao na tumeuzoea tunaamini ukikubali hadharani utaonekana dhaifu mbele ya uliyemsifu.
Ukweli ni kuwa Yanga walikubaliana na mafanikio makubwa ya Simba, hawakusimama hadharani kukiri hili ila vitendo vyao vilionesha dhahili shahiri wanayatamani mafanikio ya Simba yawe yao na pengine wawe nayo zaidi, wakakaa chini wakajiuliza nini siri ya mafanikio wakapata jibu, ni kutochungulia pesa, ndio Yanga hawainchungulii pesa wamedhamiria kupata mafanikio. Kasi waliyonayo kuelekea mafanikio ni kasi nzuri sana na pengine watawahi kufika sehemu ambayo wapinzani wao wanaiota kufika kwamiaka mingi sasa.
Yanga ni timu ambayo imekamilika kuanzia benchi la ufundi mpaka kwa wachezaji, ni timu ambayo inapambana dakika ya kwanza mpaka ya tisini, wanajitoa kwa nguvu zote ndio mafanikio yanahitaji utoe jasho na na damu.
Nadhani kwa sasa ni wakati wa wapinzani wote wa Yanga kujifunza kutoka kwao aina ya wachezaji wanaowataka na mipango yao ya michezo.
Miaka mitatu mfululizo sasa Yanga wanawashinda wapinzani wao Simba katika kuwania saini ya wachezaji wazuri hii inaonesha umakini wa hali ya juu walionao viongozi wa Yanga hii ipo wazi na haihitaji elimu mbadala kulitambua hili.
Kwa soka wanalocheza Yanga wanatoa matumaini ya kufika mbali, siwapi nafasi kubwa ya kuvuka robo fainali msimu huu ila nawapa nafasi kuwa timu ya kwanza Afrika Mashariki kufuzu nusu fainali ya klabu bingwa Afrika kwa kasi hii waliyonayo ya kuyakimbilia mafanikio.
Anaekupenda atakuambia ukweli ukweli usio pingika kuwa Simba wana mambo ya kujifunza katika kuelekea safari ya mafanikio kisoka, sio kwamba Yanga washakamilika kila idara ila wanaonesha mwanga mkubwa kuwa huko wanakoelekea watafika haraka sana kabla ya wengine.
Hongera Yanga ,
Hakika nyie ni wapambanaji wa kweli
Hakika nyie ni wapenda mabadiliko wenye nia.
Celestine Chomola [instagram officialcubicchomox]