Wikiendi hii klabu ya Yanga ilikutana na Zesco United katika mchezo wa awali wa hatua ya pili klabu bingwa Afrika. Yanga walilazimishwa sare ya goli 1-1 katika uwanja wa taifa.
- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
Karibu katika uchambuzi wa kina wa mchezo huo. Uchambuzi huu utalenga mbinu za makocha wote wawili, aina ya vikosi vilivyocheza, wapi kulikuwa na ubora zaidi na wapi kulikuwa na udhaifu, nini chanzo cha magoli yote na nini unaweza kutazamia katika mchezo wa marudiano.
VIKOSI
YANGA iliingia na viungo wanne katika eneo la kati, huku Feisal Salumu na Abdulaziz Makame wakicheza pacha kwa kwa maana kubadilishana nafasi za kiuchezaji, mmoja akipanda kuwa ‘Central Midfielder’ mwingine anabaki kuwa ‘Defensive Midfielder’.
Muda mrefu ilionena Feisal akisalia kama kiungo wa ulinzi huku Abdulaziz akiwa kama kiungo wa kati akisaidiwa na Mohamed Issa Banka aliyekuwa akishambulia kupitia upande wa kulia akitokea katikati.
Kwa upande wa ulinzi, Zahera alianza na Metacha Mnata golini, akilindwa na Mapinduzi Balama kama beki wa kulia, Ally Sonso kwa upande wa kulia, huku Kelvin Yondan na Lamine Moro wakicheza kama mabeki wa kati.
Katika nafasi ya ushambuliaji, Yanga ilianza na Sadney Urikhob kama Mshambuliaji wa mwisho na Papy Kabamba Tshishimbi kama mshambuliaji wa pili aliyetokea ndani (Inside-10).
ZESCO wao waliingia na nidhamu ya hali ya juu huku wakiendelea kuwasoma wapinzani wao Yanga. Zesco ilianza na mfumo wa 4-5-1. Kwa maana Viungo wa pembeni wawili, yaani mawinga, na viungo wawili wa Ushambuliaji na Kiungo mmoja wa ulinzi.
Yanga iliingia ikiwa na winga mmoja Asilia ambaye ni Patrick Sibomana. Sibomana alicheza upande wa kushoto, lengo la kucheza kushoto ni kumzuia Sonso kupanda sana kushambulia pia kuzuia mashambulizi ya Zesco kutokea pembeni upande wa kulia.
Mbinu hii ilifanya idadi ya mabeki eneo la Yanga kutopungua, yaani muda mwingi walikuwa watatu, Sonso, Yondani na Moro walijitanua hadi kwa Mapinduzi, pale Mapinduzi alipokwenda kushambulia.
BALAMA NA MAJUKUMU MATATU.
Mapinduzi alijibadili mara tatu kimajukumu, kwanza alikuwa beki wa kulia, Yanga inaposhambuliwa, na haya ndiyo yaliyokuwa majukumu yake ya msingi, Jukumu la pili ni kucheza kama “False full back” ilikuwa ni rahisi kumkuta Balama eneo la kati kama kiungo wa ulinzi timu inapojiandaa kufanya shambulizi, na jukumu la tatu alilolitimiza ni kushambulia kama “wingback” cha ziada alichokuwa nacho ni uwezo wa kuingia na mpira katikati ya eneo la Zesco na kuwa hatari zaidi.
Katika mechi hii Yanga walicheza kimajukumu zaidi hasa eneo lakati. Banka alitimiza majukumu mawili kwa wakati mmoja, yaani kuingia kati wakati timu inaposhambuliwa na wakati Balama alipokuwa akishambulia, hii iliongeza idadi ya watu katika eneo la hatari la Zesco.
Kwakuwa Banka sio winga kiasili, Zahera alimtumia mapinduzi kama sehemu ya kuimarisha (backup) eneo la kulia la ushambuliaji. Kwa kiasi kikubwa mbinu hii ilifanikiwa, kwani Yanga ilishambulia zaidi kupitia kulia kuliko kushoto kwa Sibomana.
TSHISHIMBI HAKUWA NA MSAADA.
Katika eneo la mbele, Sadney na Tshishimbi ndio walipewa jukumu la ushambuliaji. Sadney alitimiza jukumu lake vizuri, kwa kiasi kikubwa alijitahidi kusimama kama mtu wa mwisho japo naye kiasili sio mtu wa kusimama eneo moja. Tshishimbi alishindwa kumsaidia Sadney kama Second Striker, bila shaka Zahera aliamini Tshishimbi anaweza kubaki kama mshambuliaji, lakini Tshishimbi alishindwa kufanya hivyo.
Tatizo la Tshishimbi ni kucheza kila eneo yaani hata angekuwa kiungo, basi angecheza uwanja mzima mpaka ulinzi, tabia hii inamfanya ashindwe kutumika vizuri katika mechi zinazohitaji mipango mingi.
Kutokana na hili kuliifanya Yanga iwe na idadi ndogo ya wachezaji eneo la Zesco timu inaposhambulia, hii ndio tafsiri halisi ya viungo kupiga mashuti kutokea nje ya 18, hii ilileta faida kwa Zesco kwani mashuti mengi hayakulenga lango.
Laiti kama Tshishimbi angekuwa anasimama kama Mshambuliaji wa pili, ingekuwa ni rahisi kuwalazimisha mabeki wa Zesco kufanya makosa na kuwaadhibu. Udhaifu wa Tshishimbi ulimfanya Sadney kukabwa na mabeki watatu pindi anapojiandaa kupokea mpira na hata akiwa na mpira.
Dakika ya 25 Yanga wanapata goli baada ya Sadney kufanyiwa madhambi katika eneo la hatari. Goli hilo lilikuwa ni matokeo ya kasi ya Sadney katika kipindi cha mpito cha kushambuliwa kwenda kushambulia.
SIBOMANA KUTIMIZA JUKUMU MOJA PEKEE.
Sibomana ambaye hakuonekana kwa dakika zote, kwa maana hakuwa hatari alipokuwa na mpira lakini muda mwingi alikuwa akitimiza majukumu ya kiulinzi, kumzuia winga wa kulia wa Zesco kuingia ndani zaidi, hii ilimrahisishia Sonso kutimiza majukumu yake vizuri.
Pia inavyoonekana Sibomana aliingia akiwa na jukumu kubwa la kucheza mipira iliyokufa. Hii inathibitishwa na idadi ya mipira ya kutenga aliyoipiga. Sibomana alipiga penati na faulo zote zilizotokea katika mchezo huo.
Kwa upande wa Zesco, nidhamu yao kimchezo ilianza kupungua kila dakika zilivyozidi kuyoyoma. Zesco ilianza na viungo wengi na kumbakiza mshambuliaji mmoja mbele.
LWANDAMINA ABADILI GIA ANGANI.
Inavyoonekana George Lwandamina alikuwa akiendelea kuwasoma Yanga kwa jinsi wanavyocheza na maeneo yao yenye udhaifu. Lwandamina hakuona sababu ya kuanza na mshambuliaji mmoja kwa sababu aligundua kuwa ni rahisi kulifikia lango la Yanga.
Zesco walikuwa na mipango mingi, mipango ambayo iliwafikisha langoni mwa Yanga na kupata nafasi ya kupiga mashuti, lakini tatizo kubwa lilikuwa ni idadi ndogo ya wachezaji wao katika eneo la hatari la Yanga.
Kasi ya Zesco wakati wa kushambulia ilikuwa ndogo kiasi cha kufanya mshambuliaji wao Jesse Were kudhibitiwa kirahisi. Kumbuka Zesco ilianza na mawinga lakini walikuwa muda mwingi wakichezea ndani yaani kuubana uwanja ili kutowaruhusu Yanga kutengeneza nafasi nyingi za magoli.
Lwandamina baada ya kubaini tatizo hilo ilimbidi abadili mbinu, alimtoa kiungo Enock Subumukana na kumuingiza mshambuliaji Wiston Kalengo dakika ya 37 ili kwenda kuongeza idadi ya washambuliaji na wachezaji katika eneo la hatari la Yanga. Hii ina maana kuwa Lwandamina hakuiogopa tena Yanga, sasa alimuamua kwenda kushambulia.
Kuingia kwa Kalengo kulikuwa na tija sana kwa Zesco, kwanza timu haikupanda sana kwenda kushambulia kwani Fei toto alilazimika kuchezea chini zaidi, matokeo yake ni mechi kuwa sawa kwa pande zote.
Hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, Zesco walikuwa wakiongoza kwa mashuti ya kulenga lango na hata umiliki wa mpira. Takwimu hizi zilikuwa ni dalili kuwa Zesco wanaweza kufanya lolote kipindi cha pili.
KIPINDI CHA PILI.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, Zesco ikishambulia zaidi, Kalengo aliendelea kuwa hatari zaidi katika ngome ya ulinzi ya Yanga, alishambulia kwa kasi, aliliandama lango la Yanga. Shukrani kwa Metacha Mnata amabye alifanya kazi kubwa kipindi cha pili.
Zesco walibadilika zaidi katika eneo la kati. kipindi cha Kwanza, Thabani Kamusoko alichezea chini kwa kiasi kikubwa, lakini kipindi cha pili, Kamusoko alicheza kama wengi walivyomzoea, Box to Box Midfielder, alipanda kwa kasi kushambulia na kurudi kulinda.
Hii ilisaidia kuwasukuma washambuliaji wa Zesco na Kiungo mshambuliaji kujaa katika eneo la hatari la Yanga. Kitendo hiki kilimfanya Zahera abadili mbinu ya mchezo.
ZAHERA AFANYA MABADILIKO HEWA.
Alimtoa Sadney na kumuingiza Maybin Kalengo, pia alimtoa Banka na kumuingiza Ngasa. Mabadiliko ya kimkakati yalikuwa ni ya Ngasa, kwa maana amemtoa winga mwenye asili ya kiungo na kumuingiza winga mwenye asili ya ushambuliaji na mwenye kasi, lengo ni kumlazimisha Kamusoko na viungo wa kati, kutoisukuma Zesco katika eneo hatari la Yanga. Mbinu hii haikufanikiwa kwa sababu bado idadi ya washambuliaji katika eneo la hatari la Zesco ilisalia kuwa ndogo.
Kisha akamtoa Mapinduzi Balama, beki wa kulia na kumuingiza Ally Ally dakika ya 73. Kuingia kwa Ally Ally maana yake timu inaenda kulinda, kwa sababu beki huyu kwanza ni beki wa kati kiasili pili hana tabia ya kushambulia, maana yake idadi ya mabeki wa Yanga ilisalia kuwa sawa wakati wa kushambulia na hata kushambuliwa.
Hii iliwakaribisha zaidi Zesco katika eneo la Yanga. Yanga waliendelea kujilinda na kuchezea katika eneo lao. Zesco waliisukuma timu kwa nguvu, waliongeza kasi timu ilipokuwa inaenda kushambulia na hatimae wanapata goli la kusawazisha katika dakika za Nyongeza ikiwa ni matokeo ya Viungo wa Zesco kuisukuma timu zaidi na kumfanya Kamusoko kucheza kama box to box midfielder na kuiandikia Zesco bao la kusawazisha.
Hadi dakika tisini zinamalizika, Zesco waliongoza kwa umiliki wa mpira, mashuti yaliyolenga lango na hata ambayo hayajalenga, pia walipiga kona 6 huku Yanga wakikosa hata kona moja.
HITIMISHO.
Takwimu hizi zinatafsiri kuwa, Yanga ilianza mapema kujilinda, pia kulikuwa na tatizo katika ushambuliaji, hakukuwa na sababu ya kuanza na viungo watano, huku mshambuliaji akiwa ni mmoja pekee kwa mechi ya nyumbani.
Matokeo haya yanaifanya Yanga ikacheze mechi ngumu zaidi ugenini. Ukizingatia rekodi ya Zesco katika uwanja wake wa nyumbani. Zesco haijawahi fungwa na timu yoyote kutoka nje ya Zambia katika uwanja wake wa nyumbani, Hivyo Yanga wanahitaji nidhamu ya hali ya Juu na Kocha inabidi akaanze na washambuliaji wawili wa kati ili kuongeza idadi ya wachezaji katika eneo la hatari la Zesco pindi timu inaposhambulia.
Hii huwafanya mabeki wa Zesco kufanya makosa na hata kuwaadhibu kirahisi. Nina imani kuwa Yanga hawatotuangusha watanzania katika mchezo wa marudio.
Niambie hapo chini,
kwa mpira walioucheza Yanga unadhani
wanaweza kupata matokeo ugenini?