Mara baada ya kutupwa nje ya michuano ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) hapo jana na Singida United, kikosi cha Yanga sc kinataraji kurejea jijini Dar es salaam leo.
Yanga ilishindwa kuingia hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa kwa penati 4-2, kutoka kwa Singida United kufuatia matokeo ya sare ya kufungana bao 1-1 katika dakika 90 za kawaida.
Yanga inarejea leo ili kufanya maandalizi yao ya mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya Woloita Dicha, mchezo unataraji kupigwa siku ya Jumamosi Aprili 7, 2018 kunako uwanja mkuu wa taifa jijini Dar es salaam.
Mchezo huo ni wa mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho, ambapo Yanga wakifanikiwa kuingia hatua hiyo watavuna milioni 600 kutoka Shirikisho la soka Afrika (CAF).
Mara ya mwisho kwa Yanga kutinga hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho ilikuwa mwaka 2016.