“Mzarau mwiba Mguu huote tende”.…….huo ni usemi wa kiswahili ambao Wahenga walituachia kwa lengo la kutoa elimu ama mafunzo, juu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali kunako maisha yetu ya kila siku, pia methali ama usemi huu utukumbusha juu ya jambo lilitokea ama linalofuata ili kukabiliana nalo kwa tahadhari na umakini mkubwa
Nimeanza na methali ama usemi huo, nikiwa na lengo la kuwakumbusha tu wawakilishi pekee waliosalia kunako michuano ya kimataifa Yanga sc, mara baada ya kuwafahamu wapinzani wao katika mechi za mchujo za kuwania kutinga kunako hatua ya makundi ya kombe la shirikisho, ambapo watakutana na timu ya Woloita Dicha kutoka Ethiopia
Dicha wanaotokea katika mji wa Woloita Soddo, inashika nafasi ya nane kunako msimamo wa ligi kuu ya Ethiopia inayoshirikisha timu 16, hapa kwa mdau yoyote anaweza kuamini kuwa Yanga wana nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa kutazama ukubwa na rekodi za Yanga…..lakini katika soka ni vizuri kufanya tathimini ya kutosha kabla
Dicha ni timu inayoundwa na wachezaji wengi wa Ethiopia lakini wenye uwezo mkubwa kisoka, ikichanganya na wageni watatu ambao ni msambuliaji Arafat Djako kutoka Togo, kipa Emmanuel Obhyo kutoka Nigeria na Kiliouto Masama kutoka Chad
Na ikumbukwe kuwa Dicha kabla ya kufikia hatua hii waliiondosha Zamalek ya Misri, moja ya klabu kubwa yenye rekodi nzuri sana na utajiri mkubwa kuliko Yanga
Dicha walishinda 2-1 wakiwa nyumbani, kabla kwenda kufungwa 2-1 kule Misri kisha kuwaondosha kwa mikwaju ya penati 4-3
Pengine kwa tathimini hii tu, inatosha kuwajulisha Yanga kuwa wanakutana na timu ngumu, yenye uwezo wa kulinda na kufunga wakiwa ugenini
Hii sio njia ya mkato kwa Yanga ama wadau wengie wanavyofikiria, tena tutafanya makosa kuwaaminisha hivyo
Yanga wanapaswa kuichukulia tahadhari kubwa timu hii kwa kufanya maandalizi ya kutosha, na kuongeza umakini kutokana na ugumu wa timu wanayokutana nayo hii inaweza kuwa njia bora ya kuwasaidia kusonga mbele kunako michuano hiyo
Pengine matokeo yao dhidi ya Township Rollers kunako ligi mabingwa yanaweza kuwa somo……..lakini matokeo ya Dicha dhidi ya Zamalek wayachukulie kama funzo kwao
Kama wanafikiria ni timu wanayoweza kuitoa ni sawa lakini Je walishajiuliza ubora wa Dicha? Kama bado wakati ndio huu Aprili 6-8 sio mbali na muda hauwangoji Yanga, kutokea sasa wanapaswa kujipanga kwa mechi zote mbili ya nyumbani na ugenini
Labda nimalize kwa kusema, sina lengo la kuwatisha Yanga…….ila kalamu yangu imelenga kuwakumbusha Yanga kuwa MCHELEA MWANA KULIA HULIA MWENYEWE!