Moja ya kitu muhimu sana kuangalia katika mkusanyiko wa watu wenye tabia na rika tofauti, ni usalama kwa watu waliokusanyika. Hapo ndipo inapokuja umuhimu wa kukaguliwa kwa kila mtu anayeingia katika eneo husika kama amebeba kitu chochote ambacho kinaweza hatarisha maisha ya watu wengine katika eneo husika.
Mchezo wa soka umepitia mambo mengi sana huko duniani yanayohusu usalama, achilia mbali la mashabiki kuingia uwanjani kwenda kuwashika nyota wake. Lakini shabiki huyu kama angeingia na chupa ya soda au bia ambayo inaweza kupasuka, bila kutarajia angeweza kuitumia kumdhuru mtu pale kunapokuwa na kutofautiana. Haya kwenye mpira ya kawaida sana, hata kwenye mechi hii ya watani almanusura mashabiki wa timu moja washikane mashati.
Kwa upande fulani shirikisho lilishatangaza katazo la kuingia uwanjani na vitu ambavyo vinaweza kuwa silaha ikiwa pamoja na chupa za maji, ingawa bado mashabiki wenye hasira hutumia hata yale maji mepesi kuwarushia mashabiki au kurusha kuelekea uwanjani pindi wanapoona hawajaridhishwa na maamuzi.
Katika mchezo wa watani wa jadi ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2, klabu ya Yanga ilisambaza vipeperushi ambavyo hakika vilikuwa ni hatarishi kwa watazamaji licha ya kubeba ujumbe wenye dhumuni zuri kabisa. Vipeperushi hivi vilitengenezwa na vijiti vile vinavyotumika kuchomea mishikaki vyenye ncha kali upande wa juu.
Aina hii ya vipeperushi hakika haikuhitajika kutumika katika mkusanyiko mkubwa huu wa watu zaidi ya 50,000.
Wakati mwingine mashabiki ambao wameshika vipeperushi hivi walikuwa wakiruka juu na kutupa mikono yao juu na chini, tushukuru Mungu tu hakuna ripoti ya mtu kutobolewa macho. ‘Babu taratibu mikono hiyo umeshika kijiti hicho, utatutoboa macho‘- Shabiki mmoja wa Yanga alisikika uwanjani.
Tulijjaribu kupata maoni ya mdau mmoja ambaye pia ni shabiki wa Yanga akiijiita Dr Toyota “Wazo la Yanga ni zuri kwakuwa sasa mashabiki watajua shortcode gani ya kuchangia timu yao au kupata taarifa, ingawa huduma yao haijawa-updated, hivi vijiti lakini ni hatari. Bora wangetumia hata vile vimilija vya juice”
Ushauri wetu, bila hata kuwauliza wao kama walizingatia usalama wakati wanabuni vipeperushi hivi.
Kwa upande wa Yanga, tukiamini kabisa ni wazo zuri la kibiashara. Lakini kuna njia bora ya kutengeneza vipeperushi hivi bila kutumia vijiti vyenye ncha kali.
Kwa upande wa wahusika wa usalama wa uwanja, ni vyema pia kukawa na muongozo wa nini kinaenda kusambazwa kwa mashabiki ili kujiridhisha hakuna madhara kiusalama.
Tujaribu kufanya eneo la michezo sehemu ya furaha zaidi na kwa kuwapunguzia wasiwasi mashabiki wengine wanaotamani kuja uwanjani.