Sambaza....

Baada ya Yanga kuibuka na ushindi wa bao moja bila mbele ya Kaizer Chiefs huku bao hilo likifungwa na Kenedy Musonda msemaji wa klabu ya Yanga Alli Kamwe ameibuka na kusema jambo.

Musonda alifunga bao hilo kiufundi mbele ya kipa mzoefu wa Kaizer Chiefs Itumeleng Khune  na kumfanya Ali Kamwe kumwagia sifa “Mshambuliaji bora Kenedy Musonda, ni kama watu wanajizima data na kusahau kuwa ilimlazimu Rais Hersi Said kupanda ndege hadi Zambia kuipata saini yake,” alisema Kamwe na kuongeza.

“Ni kama watu wanajizima data na kusahau kuwa Yanga ilimpata Musonda kutoka kwenye vita kali na TP Mazembe. Ni kama watu wanajizima data na kusahau kuwa Yanga ilimsajili Musonda akiwa ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zambia [akiwa na mabao 11]. Na hapo Ligi ikiwa katikati.”

Kenedy Musonda mfungaji wa bao pekee la Yanga katika fainali ya FA.

Kamwe amewakumbushia ubora wa Musonda huku pia akiwakumbusha takwimu za nyota huyo wa timu ya Taifa ya Zambia haswa katika michuano ya CAF.

“Rafiki zangu, huyu mtu ni hatari. Ni mmaliziaji wa viwango vya juu mno. Bao lake dhidi ya  Kaizer ni ishara ya ubora wake kwenye umaliziaji. Umeziona Takwimu zake za jana kwa dakika 45? Mashuti yaliyolenga lango mawili, bao moja. Hizi Takwimu ni za mshambuliaji wa kawaida?

Tangu amekuja Yanga alilazimika kucheza kama mshambuliaji wa pembeni. Kwa wachezaji wengine hili lingekuwa jambo gumu kufanya kwa haraka na kufanikiwa, lakini Musonda alibadili nafasi yake na ni miongoni mwa wachezaji wenye takwimu nzuri zaidi kwenye Kombe la Shirikisho la CAF msimu uliopita [magoli na pasi za mabao].”

Kenedy Musonda akimuacha mlinzi wa Real Bamako katika mchezo wa kombe la shirikisho Afrika.

Msemaji huyo amekiri Yanga itatafuta mshambuliaji mwingine lakini si kwasababu ya ubora wa Musonda bali ni kumfanya kocha awe na kikosi kipana.

“Kwanini nimewakumbusha haya? Nimeona kiu ya watu kuhitaji mshambuliaji mpya kwenye kikosi cha Yanga. Ndio uongozi na benchi la ufundi ni lazima utashusha mshambuliaji mwingine pale kwa ajili ya kuongeza ushindani na machaguo mengi.

Lakini isiwe tunahitaji mshambuliaji mpya kwa sababu ya watu fulani wasiojua mpira kumchukulia poa Musonda.”


Sambaza....