Jana kwenye mitandao ya kijamii kulikuwa na habari ambayo ilikuwa inazunguka kuhusiana na Yanga kushindwa kulipa mishahara yake .
Yanga wamekanusha habari hiyo ambayo wamedai kuwa inawalenga kuwachafua wao kama wao pamoja na wadhamini wao GSM.
Mtandao wa Kandanda.co.tz ulimtafuta Afisa Habari wa klabu hiyo Hassan Bumbuli ili kuzungumzia hili suala ambalo limekuwa likienea kwa nguvu kubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Afisa Habari huyo amekanusha kuwa Yanga hakuna anayedai mishahara mpaka sasa hivi kuanzia wachezaji mpaka viongozi wa klabu hiyo kongwe nchini Tanzania.
“Tangu mwezi wa kumi na mbili mwaka jana hakuna anayedai mishahara iwe wachezaji hadi viongozi wa Yanga wametimiziwa stahiki zao”- alisema Afisa Habari huyo wa Yanga .
Pia Afisa huyo wa Habari alisema kuwa kwa sasa wako kwenye mchakato wa kuandaa mishahara ya wachezaji wa mwezi huu pamoja na mishahara ya viongozi wa Yanga .
“Kwa sasa tuko kwenye mchakato wa kuandaa mishahara ya mwezi huu kwa wachezaji pamoja na viongozi wa klabu ya Yanga , kama unavyojua tarehe 25 ndiyo muda wa wachezaji na viongozi wa Yanga kupata stahiki zao”- alisema Hassan Bumbuli.
Afisa Habari huyo amedai taarifa hizi zinakuja ili kuiodhoofisha klabu ya Yanga kuelekea katika mechi Yao ya Tarehe 8 dhidi ya Simba katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam .
“Tunajua habari hizi ni kwa ajili ya kutudhoofisha sisi kama sisi kwenye mechi yetu ya watani wa jadi dhidi ya Simba hiyo tarehe nane mwezi wa tatu , Simba wajiandae tu lazima wafe”- alimalizia Afisa Habari huyo.