WAWA ni Usajili bora kwa Simba, CHAMA ni usajili muhimu kwa Simba.
Kuna mengi sana ambayo yaliongewa baada ya Pascal Wawa kuja katika timu ya Simba. Wengi waliona Pascal Wawa umri wake umeenda sana.
Hawakuona sababu ya yeye kusajiliwa na klabu ya Simba. Dhihaka zilikuwa nyingi sana. Aliitwa babu!, hawakuamini kabisa kama anaweza akafanikiwa kucheza katika kiwango kile ambacho kilimtambulisha Wawa.
Macho yetu yaliamini Wawa ameshaisha, hana tena uwezo wa kurudi kwenye kile kiwango chake cha nyuma.
Matukio mengi sana yaliunganishwa ilimradi tu ionekane Wawa hatufanikiwa akiwa ndani ya jezi ya Simba.
Wengi walitukumbusha jinsi ambavyo alivyoshindwa kung’ara akiwa na jezi ya Azam Fc. Na wakaendelea kutukumbusha kuwa hata Sudan alishindwa kung’ara.
Mifano yote hii ilikuwa mahususi kutuonesha kuwa siku za Wawa kutundika daruga zilikuwa zimewadia. Hakuwa na uwezo tena wa kucheza soka la ushindani.
Tena katika kiwango kikubwa kama ambacho alichowahi kukicheza kipindi cha nyuma alipokuwa kijana.
Uzee wake haukuwa na thamani kubwa sana kipindi alipotangazwa kuwa mchezaji wa Simba. Wengi walihofia kasi yake kupungua.
Lakini walisahau kuwa Wawa ni mchezaji mzoefu. Na Simba ilikuwa imefuzu kushiriki michuano ya kimataifa na ilikuwa inahitaji wachezaji wazoefu.
Wachezaji ambao ni muhimu ndani na nje ya kiwanja. Hapa ndipo wengi wetu hawakuona umuhimu wa Pascal Wawa.
Na hapa ndipo kauli yangu ya kusema kuwa Wawa ni usajili bora inapoanzia. Amekuwa mchezaji-kiongozi ndani na nje ya uwanja.
Amekuwa akisimama imara kuwaongoza wenzake na wenzake wamekuwa wakimsikiliza sana kwa sababu ya uzoefu wake.
Kitu cha pili ambacho kinanifanya niamini kuwa Pascal Wawa ndiye usajili bora, Pascal Wawa amekuwa kama uti wa mgongo wa mfumo wa kocha wa Simba.
Kwanini nasema hivo? , kocha wa Simba anataka timu yake iweke mpira chini. Na anataka timu ianze kucheza nyuma.
Mabeki wa kati wahusike kwenye kuanzisha mashambulizi ya timu. Pascal Wawa amekuwa mzuri sana katika eneo hili.
Amekuwa akianzisha mashambulizi vizuri kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kupiga pasi vizuri.
Hiki ndicho kitu kizuri ambacho Simba inanufaika nacho kutoka kwa Pascal Wawa. Falsafa za mwalimu wa Simba yeye ndiye amezibeba ndiyo maana ndiye mchezaji pekee wa ndani msimu huu aliyecheza mechi zote msimu huu.
Hapa ndipo ninapoamini kuwa huu ni usajili bora sana kwa Simba. Sawa, Chama anatajwa sana na amekuwa kipenzi cha mashabiki wengi.
Na bila shaka kipaji chake hakifichiki , anakipaji kikubwa na amekuwa chachu sana ya ushindi wa klabu ya Simba kwa hivi karibuni.
Umuhimu wake unaonekana sana kwenye ubunifu kule mbele. Yeye ndiye mpishi wa magoli ya Simba na kuna wakati mwingine amekuwa akifunga sana.