Tout Puissant Mazembe (TP Mazembe) ikijulikana kama Englebert ni miongoni mwa vilabu vikubwa Afrika. Mazembe inapatikana katika mji wa Lubumbashi nchini Congo DRC. Uwanja wake wa nyumbani unafahamika kwa jina la Stade TP Mazembe unaopatikana pale Kamalondo.
TP Mazembe ilianzishwa mwaka 1939 ikijulikana kwa jina la FC Saint Georges, uwanja wake una uwezo wa kubeba jumla ya watazamaji 18,500. Rais wa klabu hiyo anafahamika kwa jina la Moise Katumbi Chapwe, miongoni mwa wanasiasa maarufu nchini Congo.
Katumbi ana historia kubwa na TP Mazembe tangu mwaka 1997 pale alipoamua kuichukua timu hiyo iliyopotea kwa miaka 18 katika uso wa kiushindani katika michuano ya kimataifa na kuisaidia kuchukua mataji mengi.
Usizikose hizi pia….
- Safari ya Yanga, Mikononi mwa Dube
- Simba na Yanga nani anaongoza kuweka mpira kwapani.
- Yanga Waweweseka! Gamondi Nje!
- Fadlu Tunaamini anawapa Ubingwa Wekundu
- Manuel Neuer ana umri sawa na uchambuzi wa soka kwa kompyuta
Chini ya Katumbi timu ilipiga hatua kubwa kwa kuwasajili wachezaji ghari kutoka kote Afrika ikiwemo Tanzania, Zimbabwe na Ghana, pia mwaka 2012 Katumbi alianzisha akademi ya Mpira wa miguu katika jimbo alilokuwa akilitumikia, jimbo la Katanga na kuwafunza mpira wakongo na kuibua vipaji vyao kwa faida ya timu na nchi.
Jina la utani la TP Mazembe ni KUNGURU licha ya nembo yao kuwa na Mamba anaemeza mpira. Klabu hii ina vingi vya kujivunia na ndio klabu yenye mafanikio makubwa zaidi nchini Congo na Afrika kwa ujumla.
Kikosi cha Mazembe kwa sasa kinanolewa na aliyekuwa kiungo nguli wa klabu hiyo, Pamphile Mihayo Kazembe. Huyu ndiye aliyekuwa kepteni wa TP Mazembe mwaka 2010, Mazembe ikifika fainali za klabu bingwa ya dunia pia alishawahi kufanya majaribio katika klabu ya Arsenal ya Uingereza.
Wakiwa nyumbani TP Mazembe huvaa jezi za rangi nyeusi kwa upande wa bukta na jezi za juu huwa ni nyeupe zenye michirizi myeusi na soksi nyeupe, wakiwa ugenini huvalia jezi za rangi ya bluu kote hadi soksi.
Mataji
Tangu mwaka 1966, TP Mazembe imekujikusanyia jumla ya mataji 24 kwa ngazi ya taifa na 11 kwa ngazi ya kimataifa. Ndio klabu yenye mafanikio makubwa zaidi nchini ikiwa na jumla ya mataji 35.
Ligi kuu.
Katika ligi yao, inayofahamika kwa jina la Linafoot, Mazembe wamebeba mara 16, yaani mwaka 1966, 67, 69, 76, 87,2000,2001, 2006, 2007, 2009, 2011, 2013,2014, 2016 na 2017. Na hii ni rekodi ambayo haijavunjwa.
Shirikisho (Coupe du Congo)
Mashindano haya, kwa Tanzania unaweza kuyafananisha na Azam Sports Federation Cup. Kwa upande wa Congo, yanafahamika kwa jina la Coupe Du Congo.
TP imebeba mara 5 mwaka 1966,67, 76, 79, na 2000 . Klabu ya DC Motema Pembe ndio klabu yenye mafanikio makubwa na kombe hili ikibeba mara 12.
DR Congo Super Cup (Ngao ya Jamii)
Hii ni mechi inayochezwa kati ya mshindi wa ligi , Linafoot na mshindi wa kombe la shirikisho, Coupe du Congo. TP Mazembe imebeba mara 3 yaani mwaka 2013, 2014, na 2016. Hii ni rekodi ambayo haijawahi fikiwa na klabu yoyote nchini Congo.
Kwa Afrika:
Klabu Bingwa Afrika. TP Mzembe imebeba mara 5 kombe la hili. Mwaka 1967, 68, 2009, 2010, na 2015. Ilibatika kuingia fainali mara mbili bila kuchukua na kuishia nafasi ya pili, hii ilikuwa ni mwaka 1970 na 1971.
Shirikisho Afrika.
Taji hili wamefanikiwa kulichukua mara 2 mfululizo mwaka 2016 na 2017. Mwaka 2013 waliingia fainali na kupoteza mbele ya Club Sportif Sfaxien ya Tunisia.
CAF Super Cup.
Hili ni kombe linalohusisha timu mbili, moja ilishinda kombe la shirikisho na ile iliyoshinda kombe la klabu bingwa Afrika kwa mwaka huo. TP Mazembe imefanikiwa kuchukua kombe hili mara 3, mwaka 2010, 2011 na 2016, na ikidunguliwa mara mbili yaani 2017 na 2018.
Na mafanikio makubwa kabisa kwa TP Mazembe katika uwanda wa kimataifa ( duniani) ni kutinga fainali ya mashindano ya klabu bingwa ya dunia mwaka 2010.
TP Mazembe ilitinga fainali za mashindano hayo maarufu duniani na kisha kufungwa na timu ya Internazionale ya nchini Italia.
Makocha.
Tangu mwaka 1979 makocha waliyoifundisha TP Mazembe ni 6 pekee ambao ni Pierre Kalala Mukendi (1979- 1981), Diego Garzitto (2003-2004), (2009-2010), Lamie Ndiaye (2010-2013), Patrice Carteron (2013-2015), Hubert Velud (2016) Pamphite Mihayo (2016- hadi leo).
Kikosi cha TP Mazembe.
Kikosi cha Mazembe kina jumla ya wachezaji 35 wenye wastani wa miaka 26, 4. Katika kikosi hicho wageni ni 12 ikiwa ni sawa na 34.3%. kikosi cha TP Mazembe kina ukwasi wa Paundi Mil. 4.12.
Katika kikosi hicho wachezaji hatari zaidi ni hawa hapa: Tresor Mputu, Jackson Muleka, Kevin Mondeko, Djo Issama Mpeko, Joseph Ochanya, Ibrahim Mounkoro, Meschak Eliya, Christian Koffi, Arsene Zola, Kabaso Chogo, Miche Mika na Rainford Kalaba.
Katika hatua ya makundi pekee, Mputu amefunga goli 3, beki Kevin Mondeko na mshambuliaji Jackson Muleka wote walifunga goli 3, kiungo fundi Meschak Eliya naye alifunga goli 2, Chiko Ushindi na Miche Mika wakifunga goli 1 kwa kila mmoja.
Kiujumla kikosi cha TP Mazembe hutegemea washambuliaji na mabeki kufunga magoli. Hii ina maana kuwa TP ni hatari zaidi kwa mipira ya kutenga na kona hasa matumizi ya vichwa. Hawa ndio TP Mazembe..
Baada ya kufuzu katika hatua ya makundi, TP Mazembe walijikuta wanaangukia katika kundi C, na huko walikutana na CS Constantine, Club Africans na Ismaily.
Walimaliza hatua ya makundi wakiwa vinara wa kundi C, wakijikusanyia jumla ya alama 11, wakishinda mechi tatu na kutoka sare mbili. TP Mazembe ndio klabu iliyomaliza hatua ya makundi ikiwa na tofauti kubwa ya mabao, magoli 9.
kipigo kikubwa zaidi walichokigawa ni kumfunga Club Africans magoli 8-0, ikipoteza kwa goli 3-0 mbele ya CS Constantine ugenini. Katika hatua ya mtoano (robo fainali) watakutana na Simba SC ya Tanzania.