Wasomaji wangu wapendwa natumaini kuwa hamjambo na kama kawaida kila mtu anaendelea na majukumu yake ya kila siku.
Kama mtakumbuka, siku chache zilizopita nilielezea mechi ya timu yetu ya Taifa, Taifa Stars dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda, Uganda Cranes, mechi ambayo nilibahatika kushuhudia pale uwanja wa soka wa St. Mary’s Kitende mjini Entebbe.
Pamoja na kuelezea mechi hiyo, nilielezea pia kuhusu uwanja huo wa shule ya sekondari ya St. Mary’s Kitende. Uwanja huu ni binafsi unaotumiwa na klabu ya Vipers FC ambayo mmiliki wake ni Rais wa zamani wa Shirikisho la soka la Uganda, Dk. Lawrence Mulindwa ambaye pia ndiye Rais wa Vipers FC na ndiye pia mmiliki wa shule hiyo ya sekondari ya St. Mary’s Kitende.
Katika makala yangu hiyo, baada ya kuuona uwanja huo nilielezea namna timu zetu pendwa za Simba na Yanga ambazo tunajinasibu nazo kuwa ndiyo miamba ya soka katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na kuwa zina “DERBY” bora kabisa kwenye ukanda huu na ambayo ni ya tatu kwa umaarufu Afrika, kwamba ndizo timu zenye mashabiki wengi zaidi kuliko mashabiki wa timu nyingine zozote katika ukanda huu. Jinsi zinavyojichelewesha sijui kwa mazoea, uzembe, ujinga au kwa makusudi kuweza kuwa na viwanja vyao bora zaidi pengine kuliko hata uwanja wa pale Kitende kwenye mji wa Entebbe, nchini Uganda.
Kwa hapa nyumbani kwa mara nyingine tena sina budi kutoa pongezi zangu kwa Azam FC, Mtibwa Sukari, Namungo FC, Mwadui FC, nafikiri na Gwambina na Geita ambao watakuwa na viwanja vyao muda si mrefu.
Timu kuwa na viwanja vyao siyo jambo la kulipuuzia hata kidogo. Narudia tena kuwa Simba na Yanga kama zitaamua na kuweka masikhara, utani, ujuha, kujifanya kujua, ujuaji mwingi na kuongea sana mdomoni kuliko matendo, basi zinaweza kuja kuwa na viwanja vizuri sana kuliko uwanja wa St. Mary’s ambao unaingiza mashabiki kati ya 15,000 hadi 25,000 huku ukiwa na VIP karibu viti 1,400. Simba na Yanga wakiamua wanaweza kuwa na viwanja hivyo ama mmojammoja ama kwa kushirikiana pamoja. Umoja ni nguvu ingawa ni timu ambazo hufanyiana mambo ya hovyo wakati mwingine lakini utawala wa timu hizi mbili ukiamua kuweka tofauti zao pembeni na zikaamua kushirikiana kwa ajili ya maendeleo ya timu zao na kuyaacha mambo ya uwanjani yaishie uwanjani basi wanaweza kuja kuwa na uwanja bora sana.
Hayo ni mawazo yangu mimi, hakuna kinachoshindikana chini ya jua!
Sasa basi nilipokuwa jijini Kampala nilishuhudia sehemu nyingi sana zilizotengwa kwa ajili ya viwanja vya michezo ikiwemo maeneo ya pale mjini kabisa ambayo ni Nakasero na Kololo. Niliona uwanja mmoja mzuri tu wa wazi pale Nakasero na Kololo. Nakasero nilishuhudia yakifanyika mazoezi jioni ile ya siku niliyowasili Kampala ambapo nilichomoka pale kituo cha basi cha Namirembe wakati namsubiria mwenyeji wangu na kuingia mtaani, lakini wakati wa kurudi pale kituo cha basi usiku ulikuwa imeingia mzee mzima nikapotea kidogo huku simu ikiwa imezima na nimeacha chaji huko kituo cha basi. Hahahaaaaaaa! 😀😀 Hii ya kupotea ina makala yake🤣🤣. Nilipotea mara mbili lakini zote ilikuwa usiku😛😛.
Vilevile katika matembezi yangu sehemu mbalimbali za nje ya Jiji la Kampala kwenye vitongoji nilikutana na shule nyingi ambazo zina vituo mbalimbali vya michezo, vingine vikiwa ni vya kulipia.
Kituo kimoja ambacho nilikikuta eneo moja linaitwa Mutungo Hill na kunifanya nibaki nimeduwaa na kushangaa katika kituo hicho kwa zaidi ya nusu saa huku nikimstaajabia mwalimu aliyekuwa akitoa mafunzo ya soka kwa watoto hao wadogo kwa umakini mkubwa huku watoto wakifuata maelekezo na mafundisho yake. Kituo hicho kinachukua watoto kuanzia miaka 4 mpaka 14 na kinafundisha michezo mbalimbali.
Baada ya kuona kituo kile pale Mutungo Hill, maswali mengi sana yalinijia kichwani na kujisemea kwamba kumbe huenda Waganda kwa muda mrefu wamekuwa wakitusumbua kwenye michezo hasa mchezo wa soka kila tunapokutana nao na wakati mwingine wakitufunga nje ndani hii labda inatokana na wao kuanza kuwekeza kwenye michezo kwa watoto wadogo toka wakiwa kwenye umri mdogo sana na inasemekana kuwa nchini Uganda, michezo ni lazima mashuleni na ni sehemu ya masomo katika mitaala yao. Hata wakati nikiwa nchini humo niliona kwenye vyombo vya habari Waziri wa michezo akiwaaga wanafunzi 400 kama sijakosea waliokuwa wanakwenda Arusha kwenye michezo ya shule za Afrika Mashariki. Kwa idadi kubwa kama hiyo inaonyesha ni kwa namna gani wenzetu wanaipa michezo kipaumbele kwa kuanza kuitilia mkazo wakati bado wakiwa kwenye ngazi za chini kabisa na hii imekuwa ikiwasadia sana.
NINI CHA KUJIFUNZA?
Kwa namna nilivyoona kwa wenzetu Waganda walivyojikita kwenye kuendeleza michezo toka kwenye hatua ya awali kabisa basi hata sisi tukiamua inawezekana kabisa. Tukaanzisha vituo vingi sana vya michezo kwa ajili ya watoto wa kuanzia umri kama wa wenzetu na kuendelea kwa nchi nzima, kwa kufanya hivyo na kwa kuweka mikakati, miundombinu, na uwezeshaji basi tunaweza kufanikiwa na kuja kuyaona matunda ya uwekezaji huu kwenye michezo jatika miaka michache ijayo.
Mwalimu Nyerere alipata kusema hivi:
IT CAN BE DONE PLAY YOUR PART!, THUS, IT CAN BE DONE LET US PLAY OUR PART!
Kabisi ka ndagala!
Pichani ni picha nne, tatu ni za kawaida na moja ya video ambazo nilizipiga wakati nikistaajabia mafundisho ya mwalimu wa soka wa Kiganda katika kituo hicho kilichopo barabara ya Mutungo Hill, barabara ambayo ni maarufu kama Mutungo Ring Road ambapo ukiifuata barabara hiyo ya mzunguko, kwa kuizunguka japo ni ndefu, utafika mpaka kwenye miji ya Port Bell na Luzira mahali lilipo ziwa Victoria jijini Kampala ingawa kuna njia za mkato kuweza kufika ziwa Victoria kwa kuukatisha mlima huo wa Mutungo au kwa kufuata barabara ya Port Bell pale maeneo ya Kitintale wenyewe Waganda wanatamka Chitintale!