Sambaza....

Mkongwe, fundi pia wa mpira. Kipindi chake ambacho damu yake ilikuwa ya moto ilikuwa ngumu kwa jicho la mwanadamu yeyote yule kufurahia kumuona akishika mpira.

Huyu ndiye mmoja wa binadamu ambao waliwekewa komputa ya mpira wa miguu katika ubongo wake. Ubongo wake ulikuwa na vingi sana vya kuonesha.

Miguu yake iliongozwa na ubongo wake, miguu yake ilifanya mahesabu magumu ya mpira wa miguu. Mahesabu ambayo miguu mingi ilikuwa inashindwa.

Ni hesabu gani ambayo miguu ya Haruna Moshi “Boban” haikufanyika kwenye miguu yake ?.

Labda tu hukuwahi kubahatika kumtazama. Kama uliwahi kumtazama utakubaliana na Mimi kwenye hili. Utakubaliana kabisa huyu ni mmoja wa mafundi ambao waliwahi kuzaliwa kwenye ardhi yetu kwa ajili ya kuujenga mpira wa miguu.

Kwa ajili ya kuufanya mpira wa miguu kuonekana ni sehemu yenye burudani, sehemu ambayo ilikuwa inavutia sana kutazamika kwa macho.

Ndiyo maana ufundi wake ulifanikisha kujenga jengo tamu la mpira wa miguu. Jengo hili alilijenga katika ardhi ya msimbazi, ardhi ambayo inamiliki klabu ya Simba.

Hii ndiyo ardhi haswa ambayo ilifanya dunia ya mpira wa miguu imtambue vizuri Haruna Moshi “Boban”.

Alikuwa mfalme kipindi chake. Ufalme ambao hata hawa wakina Chama hawajafikia bado. Alikuwa anakubalika, alikuwa anapendeka sana.

Unajua kwanini ?, hii ni kwa sababu alitufanya tufurahie kutazama mpira hasa hasa kila miguu yake ilipokuwa inashika mpira.

Alikuwa na kila aina ya sababu ya kuitwa mchezaji bora kwa kipindi hicho. Alikuwa na kila sababu ya kuitwa FUNDI wa mpira.

Alijua kupiga pasi vizuri, alijua kutengeneza nafasi za kufunga magoli vizuri. Alijua kufunga pia magoli. Alijua kuupaka rangi ya kila aina mpira.

Kwa kifupi alikuwa mchezaji ambaye amekamirika sana tena sana. Dhambi pekee ambayo aliifanya kwenye ulimwengu huu mpira wa miguu ni yeye kutofika sehemu ambayo kina Mbwana Samatta wapo.

Hii ni dhambi kubwa sana ambayo itamhukumu kwa kipindi kirefu sana , alistahili kucheza nje. Tena kwenye ligi nzuri inayolipa vizuri.

Hakuna mwanadamu ambaye angekataa kulipa pesa yake kwa ajili ya kwenda kushuhudia burudani inayotokana na miguu ya Haruna Moshi ” Boban”.

Kipindi chake kucheza Simba kiliisha. Akawa amepotea na akapisha kizazi kingine kipya. Kizazi ambacho kilikuwa na changamoto mpya.

Kizazi ambacho kilitufanya tuone Haruna Moshi “Boban” kama amepotea kwenye uso huu wa mpira wa miguu.

Tulijua amepotea. Tulijua kabisa ameshastaafu soka. Na wengi wetu tulitambua kuwa yuko katika timu za “Veteran”.

Huku ndiko sehemu pekee ambayo tuliamini tunaweza kumpata Haruna Moshi ” Boban”. Na hii ni kwa sababu moja tu , tuliamini nyakati zake zimeshapita.

Zile zama za Haruna Moshi “Boban” kuonekana kama Mfalme wa Kariakoo tulikuwa tunaamini zimeshapita kabisa.

Cha ajabu African Lyon walituletea tena Haruna Moshi “Boban” katika uso wa mpira wa miguu. Kwa mara nyingine tuliatamani kabisa kuona kama yaliyokuwemo kipindi cha nyuma bado yamo?

Hii ndiyo ilikuwa kiu yetu kubwa sana kwa kipindi hicho. Mboni za macho yetu zilikuwa makini sana kumtazama vizuri Haruna Moshi “Boban”.

Alionekana kama mchezaji ambaye anatamani sana kucheza. Ile komputa yake ya mpira wa miguu ilikuwepo bado, lakini hakukuwepo na umeme wa kuifanya iwake na kuonesha data.

Mwili ulikuwa unapingana na vitu vingi sana kwa Haruna Moshi ” Boban”. Lakini Yanga sijui walitaka kutuaminisha kuwa bado Haruna Moshi “Boban” bado ni yule wa kipindi kile?

Kitu hiki wameshindwa mpaka sasa hivi kutuaminisha. Haruna Moshi “Boban” hana kasi tena kama kipindi kile cha nyuma.

Hana tena uwezo wa kufanya chochote bora kama kipindi kile. Muda wake umeshapita na alikuwa na bahati kubwa sana kusajiliwa na Yanga kipindi hiki.

Na Yanga wamemsajili Haruna Moshi “Boban” kwa sababu tu wanapitia kipindi kigumu katika masuala ya uchumi.

Hawana nguvu tena kubwa ya kuingia ndani ya soko na kupigania mchezaji ambaye anaonekana bora kama ambavyo walikuwa zamani.

Hawana uwezo kukidhi mahitaji ya mchezaji bora kwa sasa na mahitaji ya soko la wachezaji wa sasa, ndiyo maana wanafikia hatua ya kuangukia kwa Haruna Moshi “Boban”.

Mchezaji ambaye hana uwezo mkubwa wa kuisaidia Yanga kwa sasa.Mchezaji ambaye anaonekana amekuja kula pension yake tu pale Jangwani.

Sambaza....