Sambaza....

Timu ya Taifa ya Tanzania “Taifa Stars kesho itashuka dimbani kuvaana na Uganda “The Cranes” katika tiketi ya kufuzu fainali za Afcon 2023 zitakazofanyika nchini Ivory Coast. Mchezo huo utapigwa saa mbili usiku katika Dimba la Benjamin Mkapa.

Tayari Stars ina alama nne baada ya kutoka kumfunga Uganda ugenini, sare dhidi ya Niger ugenini na walifungwa na Algeria nyumbani. Hivyo wanashika nafasi ya pili nyuma ya Algeria wenye alama tisa.

Kuitwa kikosi kwa walinzi wa pembeni wa Simba Mohamed Hussein na Shomary Kapombe na kuumia kwa Himid Mao huenda kukamlazimisha mwalimun Adel Ameouche kubadili kikosi chake kuelekea mchezo huo wa marudiano dhidi ya The Cranes.

Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Adel Amrouche

Ni wazi mwalimu ataingia na mfumo ule ule wa walinzi wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu  mbele kama ambavyo alivyoanza mchezo uliopita dhidi ya Uganda ugenini lakini safari hii ataamua kushambulia zaido tofauti na kulinda sana. 

Kuumia kwa Himid Mao Mkami ambae mchezo uliopita alicheza pacha na Mzamiru Yassin katika kiungo cha ulinzi ni wazi kutamfanya  kubadili mipango yake kwa kumuingiza kikosini Mohamed Hussein Tshabalala acheze mlinzi wa kulia halafu Novatus Dismas alieanza kama mlinzi wa kushoto acheze katika eneo lake la kiungo wa ulinzi. 

Pia katika eneo la ushambuliaji ni wazi mwalimu Adel atahitaji kasi zaidi na hivyo mshambuliaji Said Hamis huenda akampisha Abdul Sopu  katika washambuliaji watatu juu ili kutimiza mfumo wa 4:3:3  ama 4:2:3;1 ambapo ataungana na Simon Msuva pamoja na Mbwana Samatta.

Mshambuliaji wa Taifa Stars Said Hamis akipiga krosi mbele ya mlinzi wa Uganda

Eneo la ulinzi haswa katikati halitoathirika sana na watasimama walewale Ibrahim Bacca pamoja na Bakari Mwamnyeto wakati ulinzi wa kulia mwalimu ataamua aanze na yuleyule Dickson Job ama kama atataka kushambulia zaidi basi Dickson Job atampisha Shomary Kapombe. 

Katika mchezo huo ambao ili Stars iweze kuweka matumaini yake hai ni lazima wapate ushindi dhidi ya Uganda na kuwafanya kufikisha alama 7 ambazo zitawafanya kuhitaji alama tatu pekee katika michezo miwili iliyosalia bila kujali matokeo yawapinzani. 

Niger ana alama mbili na Uganda wana alama moja ambao ndio washindani wakubwa wa Stars katika nafasi ya pili hivyo Stars akishinda leo na Niger akifungwa na Algeria ni wazi tutakua tumepiga hatua moja kuelekea Ivory Coast. 


Sambaza....