Janga la corona likiwa bado ni kizungumkuti cha dunia na kuendelea kusimamisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi pia kwenye mpira wa miguu hali ni tete. Ikiwa haifahamiki ni lini ugonjwa huu utaisha na mpira kuendelea tena kuchezwa kama kawaida tayari kuna msukumo wa kumaliza Ligi ili timu zote za Ligi Kuu na madaraja ya chini zijue nafasi yao katika msimu ujao.
Tayari Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetoa waraka likiwataka washirika wake watoe uamuzi wa ligi zao ifikapo Mei 5 mwaka huu. Baadhi ya nchi tayari zimetoa maamuzi ya Ligi zao huku mashirikisho ya soka yakizifuta Ligi zao na kutoa maamuzi mezani. Nchi kama Guinea na Kenya wao hivi karibuni wamemaliza ligi zao na kutoa maamuzi ya bingwa na timu zitakazoiwakilisha nchi.
Kwa Ligi Kuu Bara mpaka sasa Shirikisho la Soka na Bodi ya Ligi hawajatoa maamuzi yoyote huku wakisubiri serikali kutoa muongozo kwanza wa usalama wa afya kama nchi(Kabla ya jana Mh. Rais kuongea na vyombo vya habari) ili kuona nchi ipo salama kiasi gani kiafya ndipo uamuzi ufanyike.
Katika msimu huu wa 2019/2020 Ligi yetu timu zinatakiwa kupungua kutoka timu 20 mpaka kubaki timu 16 hivyo basi timu zitakazoshuka moja kwa moja mpaka daraja la kwanza ni nne na nyingine mbili kucheza “Playoff” na timu za daraja la kwanza. Kwa maana hiyo watakaoshika nafasi ya 20,19,18 na 17 watashuka moja kwa moja mpaka daraja la kwanza na watakaoongoza kundi A na B wa daraja la kwanza watajikatia tiketi ya kucheza VPL msimu ujao wa Ligi.
Watakaoshika nafasi ya 16 na 15 watacheza “Playoff” na washindi wapili wa kila kundi kutoka Kundi A na B wa daraja la kwanza.
Nani apande nani ashuke ligi ikisitishwa?
Kutokana na msimu huu kutakiwa kushusha timu nyingi ni vyema timu nne (20,19,18 na 17) zikashuka moja kwa moja na timu mbili za za FDL zikapanda moja kwa moja.
Timu 18 VPL
Ligi ya msimu ujao ingechezwa kwa kishirikisha timu 18 badala ya 16 kama ambavyo imepangwa na TPBL na TFF. Kwa maana hiyo timu nne za mwisho zingeshuka daraja na timu mbili zinazoongoza makundi za FDL zingepanda moja kwa moja.
Playoff ambayo ingetakiwa kushirikisha timu za VPL na FDL zingefutwa na hivyo watakaoshika nafasi ya 16 na 15 VPL na watakoshika nafasi ya pili kila kundi FDL hawatokutana.
TFF kukubaliana na Vodacom ambae ndie mdhamini mkuu wa Ligi
TFF pamoja na Vodacom wangekaa na kukubaliana kutumia busara na kuamua kubakisha timu 18 kwa msimu ujao wa 2020/2021 wa VPL. Kwa maana hiyo kutakua na ongezeko la timu 2 kutoka kwenye ile bajeti ya udhamini wa timu 16, hivyo Vodacom na TFF wangejaribu kufanikisha kuongeza bajeti ya hizi timu mbili.
Lakini pia TFF wangeweza kutafuta chanzo kingine cha mapato kutoka kwa wadhamini wenza (KCB Bank) ama wadhamini wakuu (Azam tv)wa ligi ili kuweza kuzihudumia hizo timu mbili.
Bingwa wa Ligi
Mpaka ligi inasimama Simba alikua na alama 71 katika nafasi ya kwanza huku akifwatiwa na Azamfc mwenye alama 54 katika nafasi ya pili.
Kwa kufuata msimamo huo Simba angekabidhiwa ubingwa wa VPL kwa kufuata msimamo wa Ligi na kufwatiwa na timu zingine kama zinavyofuata kuanzia nafasi ya kwanza mpaka ya mwisho
Nani kuiwakilisha nchi?
TFF ingefuata msimamo mpaka ambapo Ligi ikiwa inasimama ambapo Simba akiwa nafasi ya kwanza angekwenda kushiriki Klabu Bingwa Afrika na Azam fc wanaoshika nafasi ya pili wangeshiriki kombe la Shirikisho barani Africa.