Bila shaka ameshafanikiwa kushika nyoyo za mashabiki wa Simba. Hili halina ubishi kwa sababu alifainikwa kwa kiasi kikubwa kuwapa ambacho kilikuwa burudani kwao. Aliwapa ushindi mkubwa!, hii ndiyo ilikuwa furaha ya mashabiki wa Simba.
Timu ilicheza soka la kuvutia, kitu ambacho kwa mashabiki wa Simba ni kama utamaduni wao. Kwao wao kucheza mpira wa kuvutia tena timu ikiwa inashinda magoli mengi hiyo ndiyo jadi yao.
Hapa ndipo Masoud Djuma alifanikiwa kuwakamata , na aliwakamata haswaa mashabiki wa Simba!. Hata maisha ya Pierre Lenchantre yalikuwa mafupi pale Simba na kibaya zaidi Pierre Lenchantre alikuja akawa kwenye kivuli cha Masoud Djuma kwa timu kucheza mfumo wa 3-5-2.
Mfumo ambao kwa mashabiki wengi wa Simba walikuwa wanauamini ndiyo mfumo bora na imara ambao unaweza kuwapa ubingwa. Kitu ambacho kilikuwa sahihi kwa kipindi hicho kwani Simba walifanikiwa kubeba ubingwa chini ya huo mfumo.
Maisha ya msimu uliopita yaliisha, yakatakiwa kujengwa maisha mapya, nayo ni maisha ya msimu huu. Maisha ambayo yalimlazimu Pierre Lenchantre atoke na kumpisha Patrick Assumes. Wakaajili kocha mpya tena , kocha ambaye bila shaka alihitaji muda tena kutengeneza aina ya timu ambayo anaitaka yeye. Kocha ambaye asingefanya kama Pierre Lenchantre alivyofanya kwa kutembea kwenye kivuli cha Masoud Djuma.
Hivo ilihitajika muda kwa timu kuendana na mfumo ambao kocha mpya anautaka. Siyo kitu cha siku moja kwa kocha kupata timu ambayo anaitaka.
Nipo najaribu kuwaza utofauti wetu na watu wa dunia ya kwanza. Nimewaza sana utofauti wetu na wao ni wapi unaanzia. Nimejaribu kuwatazama Patrick Assumes kocha wa Simba na Unai Emery kochwa Arsenal ambao wote mpaka sasa wamecheza mechi tano (5) za mashindano.
Kuanzia kwenye mechi ya ngao ya jamii mpaka kwenye mechi ya Leo dhidi ya Mbao , Simba kacheza mechi tano na kafungwa magoli mawili tu na akifunga magoli matano (wastani wa goli moja kila mechi). Hii inaonesha Simba wana ukuta imara, kitu ambacho Patrick Assumes amefanikiwa, ila hawana safu Kali ya ushambuliaji kama ya msimu uliopita(tatizo ambalo linaweza kurekebishika).
Na katika hizo mechi tano , Simba kafungwa mechi moja, katoa suluhu mechi moja na kashinda mechi tatu. Matokeo ambayo ni mazuri yenye asilimia 95% za ushindi tena chini ya kocha mpya ambaye ndiyo anatumia muda huu kutengeneza aina ya timu anayoitaka yeye.
Hii ni kama ilivyo kwa Unai Emery ambaye ana timu mpya ya Arsenal ambapo anatumia muda wake kutengeneza timu kulingana na mbinu zake. Ameiongoza Arsenal katika mechi tano (5) kama ambavyo Patrick Assumes (mechi ambazo ni za mashindano). Na katika hizo mechi tano kafungwa mechi mbili na kushinda mechi tatu, huku akiruhusu magoli Tisa (hii inaonesha ukuta wake ni mbovu).
Utofauti wa mashabiki wa Simba na Arsenal unaanzia hapa!, Mashabiki wa Arsenal wanaamini katika hatua, wanaamini hatua ndizo husababisha kujenga kitu imara. Wana Uvumilivu, wanajua mafanikio ya kupata timu imara hayaji siku moja ndiyo maana wengi wa mashabiki wa Arsenal wamempa muda Unai na hutosikia kabisa kelele nyingi za kuchoka na Unai ndani ya mechi tano tu!, lakini huku kwetu ni tofauti.
Tulianza kumchoka Patrick Assumes siku ile tu anatambulishwa na siku ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ndiyo tulimchoka zaidi.
Kwa kifupi tofauti yetu na wao ni moja tu, ipo kichwani ndiyo maana tunakosa kumvumilia Assumes na tumeamua kuitumia fimbo ya Masoud Djuma kumchapia.