Sambaza....

Mwisho wa kila safari huwa kuna funzo kubwa ndani yake, na binadamu siku zote huimarika na kuwa bora kupitia mafunzo tunayoyapata katika safari zetu kwenye maisha.

Safari ya michuano ya kombe la nchi wanachama wa Afrika Mashariki (CECAFA) iliisha jana kwa kushuhudia Kenya ikichukua kombe lile.

Kenya kuchukua kombe lile haikuwa habari kubwa na ya kushangaza sana, lakini Zanzibar kufika fainali ya michuano hiyo ilikuwa habari kubwa na ya kushangaza.

Timu ambayo ilikuwa imesubiri miaka 22 kufika fainali ya michuano hii, ambapo mara ya mwisho kufika ilikuwa mwaka 1995.

Image result for Zanzibar Heroes

Muda mrefu ulikuwa umepita huku Zanzibar akisubiri kwa hamu siku hii, kukaa kwake muda mrefu bila kufika fainali ya kombe hili ndiko kuliwapa watu moja ya sababu ya Zanzibar kutokufanya vizuri.

Kikosi cha Zanzibar hakikuwa kimesheheni nyota wengi wa majina ya kutisha ambayo yangetumika kuogofya timu zingine.

Lakini walikuja na wachezaji wenye majina ya kawaida, hali ambayo iliwafanya wapinzani wao kuiona Zanzibar kama timu ya kawaida.

Wakaiweka kwenye ukawaida, hawakuipa nafasi kubwa ,wakaipa nafasi ya kawaida.

Zanzibar ikakubali kuwa timu ya kawaida ikaingia na faida ya kuitwa timu ya kawaida.

Faida hii iliwanufaisha sana wao kwani timu nyingi ziliingia zikiamini Zanzibar ni underdog, hivo timu zikiingia zikiwa zimejiamini sana mbele ya Zanzibar.

Zanzibar iliingia kawaida, ikiwa haijiamini sana kama timu zingine, hali ambayo iliifanya icheze mpira ikiwa katika hali ya utulivu, hali ambayo iliifanya wafanye maamuzi mazuri ambayo yalikuwa na manufaa kwao.

Utulivu wao uliwafanya wacheze bila presha na kutumia vizuri nafasi ambazo walikuwa wamezitengeneza.

Mfano katika mechi ya fainali, walitanguliwa na wenyeji Kenya mara mbili, lakini hawakuonekana kuwa na presha, ila walitulia na kutengeneza nafasi ambazo ziliwasaidia kusawazisha magoli yale.

Moja ya timu ambazo zilikuwa zinapewa posho ndogo, Zanzibar ilikuwa moja wapo.

Lakini kwao posho kubwa lilikuwa siyo jambo la mbele, kitu ambacho ƙkilikuwa mbele zaidi kwao ni maslahi ya Taifa lao.

Nchi yao ilikuwa kila kitu kwao kuliko kitu kingine, waliamua kuipigania nchi yao katika ardhi ya ugenini.

Manung’uniko ya posho ndogo kwao hayakuwepo, kitu pekee kilichokuwepo katika kichwa chao ni wao kujitengeneza wawe mashujaa wa nchi yao.

Image result for Zanzibar Heroes

Mashujaa ambao wataimbwa, watasomwa kwenye vitabu vya mashujaa, ndiyo maana walipigana kwa nguvu na kwa pamoja bila kuchoka kuhakikisha nchi yao ikipata ushindi.

Walipigana katika mazingira magumu kuhakikisha wanaipata furaha, jasho lao lilikuwa muhimu kwa nchi yao kuliko kitu chochote.

Waliamua kuitumikia nchi yao na kuachana na dhana ya kuitumikia pesa, uzalendo ulikuwepo ndani yao.

Hii imekuwa tofauti sana katika kikosi cha timu yetu ya Taifa, timu ya taifa wachezaji wake hawachezi kwa uzalendo licha ya kupewa posho vizuri kama motisha lakini uzalendo ndani yao wanakosa.

Hata kipindi ambapo huwa wanakuwa “underdogs” huwa wanatoka mchezoni kwa kukubali kufungwa kabla hata mechi haijaanza.

Lakini Zanzibar imetupa somo ambalo tunatakiwa kulichukua na kutembea nalo kwa ajili ya manufaa ya mpira wetu .

Sambaza....