Sambaza....

Tunarudi kule kule ambako tumewashawahi kupitia na kwa bahati mbaya sana hatukufanikiwa kupata kitu ambacho ni bora. Tuliamini katika kamati ya kusaidia timu mbalimbali kushinda lakini mwisho wa siku timu zetu zilikuja na matokeo ambayo siyo rafiki.

Ni jambo ambalo siyo la kuficha kabisa kuwa hizi kamati za kusaidia timu zetu kushinda zimekuwepo kwa muda mrefu na bado tunaendelea nazo lakini hakuna mafanikio tuliyopata. Kwenye kipindi cha Marcio Maximo, kipindi cha mhemko, kipindi ambacho wimbi kubwa la watu kuipenda Taifa Stars lilikuja.

Na kipindi hicho tuliunda kamati ya kutufikisha Afcon na kufuzu kombe la dunia lakini mwisho wa siku hatukupata kitu chochote, kwanini hatukufuzu ?, jibu jepesi tu hatukuwa na kikosi bora cha kutufikisha huko. Sawa tulifanikiwa kupata nafasi ya kuingia CHAN mashindano yanayoshirikisha wachezaji wanaocheza timu za ndani.

Sibezi mafanikio haya, lakini hayakuwa makubwa kiasi kile ambacho tulikuwa tunakitegemea sisi. Lengo letu kubwa ni Afcon na kombe la dunia.

Muda ukaenda, tukawa tunazidi kuwa na kamati mbalimbali ambazo pia lengo kuu ni kuifanya Taifa Stars kushinda ili ifuzu michuano mikubwa ya kimataifa.

Lakini mwisho wa siku hatukuweza kufuzu kwenye michuano hiyo zaidi ya kupata aibu tu kila uchwao, yote haya ni kwa sababu moja tu hatukuwa na kikosi cha kutufikisha huko.

Jamal Malinzi alitupatia Serengeti Boys iliyoshiriki Afcon ya vijana kule Gabon mwaka 2018. Kukawepo na kampeni ambayo ilianzishwa na kamati maalumu ya Serengeti Boys.

Naikumbuka sana kampeni hiyo ya Gabon mpaka kombe la dunia. Tulihitaji kufika nusu fainali tu kwenye michuano hiyo ya Afcon ili kupata nafasi ya kufuzu kombe la dunia ambalo lilikuwa linafanyika India.

Kamati iliundwa, ikaja na kampeni kubwa na mahususi. Lakini mwisho wa siku hatukufanikiwa kufuzu kombe la dunia. Hii ni kwa sababu tu hatukuwa na kikosi cha kutufikisha huko.

Naamini kuna kamati nyingi sana ambazo zimeundwa lakini hazipishani sana matokeo. Matokeo ni yale yale hakuna kamati ambayo imefanikiwa kuifanya timu yoyote ya Taifa kufika sehemu ambayo tunaota.

Leo hii pia imeundwa kamati ya saidia Taifa Stars kushinda kuelekea katika mechi ya Uganda itakayochezwa mwezi ujao. Mechi ya kufuzu Afcon, tunapitia kwenye njia zile zile ambazo hatukufanikiwa. Njia zile zile ambazo hazikutupa suluhisho la tatizo letu kimpira.

Simaanishi kuwa Taifa Stars inaenda kupoteza mchezo dhidi ya Uganda kwa sababu ya kamati hii ya saidia Taifa Stars kushinda. Sina maana hiyo kabisa. Ila hata kama Taifa Stars ikishinda bado tatizo letu litakuwa lile lile , tutakuwa bado hatujalitibu kabisa. Nakupeni mfano mdogo tu, baada ya Marcio Maximo kutupeleka CHAN je tulifanikiwa kufuzu tena?

Jibu ni hapana , kwanini ?, kwa sababu hatukuandaa kizazi kingine ambacho kingetupa mwendelezo mzuri wa kufuzu kwenye michuano ya kimataifa.

Na ndicho kinachoenda kutokea baada ya hapa. Tunaweza kumfunga Uganda, tukafuzu kabisa michuano ya Afcon lakini tukakosa mwendelezo wa kufuzu kwa sababu ya kukosa kizazi kingine cha kuendelea kufuzu.

Hapa ndipo palipo na suluhisho, na hapa ndipo ambapo tunapakwepa kwa kurukia sehemu ambayo hatujafika kabisa.

Kwenye ukuaji lazima kuwepo na hatua ya ukuaji mpaka pale mtu atakapokuwa ameonekana amekomaa.

Sisi bado hatujakomaa kabisa lakini tunalazimisha tukomae. Hapa ndipo tunaposhindwa kufanikiwa na kamati zetu.

Mimi nina kitu kimoja tu ambacho binafsi nakiona ni bora. Hizi kamati ambazo zinaundwa kila uchwao kwa ajili ya kusaidia Taifa Stars kushinda , ziundwe kwa malengo mengine.

Siyo dhambi kabisa kurudi kwenye njia sahihi. Kwanini hizi kamati za kusaidia Taifa Stars kushinda zisiwe mahususi kwa ajili ya kujenga vituo vya kulea, kuibua na kukuza vipaji vya mpira?

Kwa mfano kukawa na kampeni ya kujenga Taifa Stars imara ijayo. Ni ukweli ulio wazi kuwa Taifa Stars ijayo imara itapatikana kwa kujenga kizazi imara. Kizazi ambacho kitatokana na kuwa na vituo vikubwa. Mfano tu, kukawa na wazo la kuwa na kikubwa kwa kila kanda.

Mfano, Kukawa na kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji katika kanda ya ziwa, kingine kikajengwa kanda ya kaskazini. Kingine kingajengwa kanda ya kati, kingine kikajengwa kanda ya mashariki na cha mwisho kikawa kanda ya nyanda za juu kusini.

Kila kituo kitahudumia mikoa ya kanda husika. Hizi itasaidia sana kuibua, kukuza na kulea vipaji vya watoto. Faida yake nini ?, kuwa na timu imara za Taifa kuanzia timu za vijana. Ambazo zitakuwa na mwendelezo wa kushiriki michuano ya kimataifa tangu wakiwa watoto.

Watoto hawa watakuwa wamefundishwa misingi bora ya mpira wa miguu. Hawa vijana wakiwa wanashiriki michuano ya vijana tangu wakiwa watoto itatusaidia kupata timu imara ya Taifa ya wakubwa.

Yani kijana akawa ameshiriki michuano ya Afcon ya vijana kuanzia ya chini ya umri wa miaka 17, 20, 23. Afu akashiriki michuano ya Olympic , jumuiya ya madola huyu akija kuingia timu kubwa ya Taifa atakuwa na msaada mkubwa.

Kwa sababu tu presha kubwa ya michuano ya kimataifa anakuwa ameshaizoea tangu akiwa kijana. Yani kajengwa kuwa mshindani tangu akiwa kijana.

Yani huyu haina haja ya kumuundia kamati ya saidia Taifa Stars kushinda. Mabingwa wa Afcon mwaka 2018 ambapo na sisi tulishiriki (Mali) wiki iliyopita wameshinda Afcon ya chini ya miaka 20.

Wachezaji waliochukua Afcon ya chini ya miaka 20 wachezaji nane wa kikosi cha kwanza walikuwepo kwenye kikosi kilichoshinda Afcon ya vijana chini ya miaka 17.

Hawa Mali kupitia hawa vijana watakuja kuwa na timu ya Taifa ya wakumbwa imara kwa sababu ya hawa vijana. Hebu tuachaneni na siasa za kuunda hizi kamati ambazo hazijawahi kutupa suluhisho la tatizo letu.

Tuache kupoteza muda wa kamati hizi ambazo siyo tabia ya ugonjwa wetu. Tufikirieni namna ambavyo tutakavyounda kamati ya kusaidia tuwe na Taifa Stars imara ijayo. Kamati ambayo itatusaidia kuhamasisha watu ili tupate vituo vitano kutoka kila kanda iliyopo hapa Tanzania kwa manufaaa mapana ya Taifa letu.

Sambaza....