BONDIA namba moja nchini, Tony Rashid anatarajia kupanda ulingoni kutetea mkanda wake wa ubingwa wa Afrika dhidi ya Sabelo Ngebinyana raia wa Afrika Kusini katika pambano litakalopigwa Februari 24, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es salaam.
Tony atapanda ulingoni kutetea mkanda wake huo katika pambano lililoandaliwa na Kampuni ya Kemmon Sporty Agency chini ya Mkurugenzi wake Saada Salum ambaye ni promota wa pambano hilo ambalo pia Seleman Kidunda atapanda ulingoni kuwania mkanda wa ubingwa wa Afrika ABU dhidi ya Patric Mukala katika pambano ambalo litakuwa ndilo ‘Main card.”
Tony mwenye mwenye nyota tatu na nusu akiwa na rekodi ya kucheza jumla ya mapambano 18 akiwa ameshinda 14 kati ya kumi ni kwa KO huku akipoteza mapambano mawili kati ya hayo moja likiwa ni kwa KO na kutoka sare mapambano mawili wakati mpinzani wake Sabelo Ngebinyana mwenye nyota tatu na nusu akiwa amecheza mapambano 21 kati ya hayo ameshinda 15, 11 ikiwa ni KO na amepoteza mapambano sita huku moja likiwa ni kwa KO.
Promota wa pambano hilo kutoka Kemmon Sport Agency, Saada Salum alisema katika mapambano kumi waliokuwa nayo awali wameamua kuliongeza na pambano la Tony ambaye atakuwa na kazi ya kutetea mkanda wake wa ubingwa ABU dhidi ya Sabelo Ngabinyana kutoka Afrika Kusini hali iliopelekea kuwepo kwa mapambano mawili ya ubingwa wa ABU kwenye pambano hilo.
“Maandalizi ukweli yanaendelea vizuri ingawa wito wetu bado upo kwa wadhamini kuendelea kujitokeza kwa sababu hili pambano kubwa kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania kutokana na mambondia wawili wa Tanzania kuwania mikanda ya ubingwa wa Afrika ABU ambayo ndiyo mkanda mkubwa wa ubingwa kwa Afrika.
“Najua wengi walitegemea kumuona Kidunda peke yake lakini kama Kemmon Sports Agency tumeamua kumuongeza Mtanzania mwengine, Tony Rashid lakini yeye atatetea mkanda wake wa ubingwa aliomchapa Bongani Mahlangu mwaka jana hivyo tunaamini siku hiyo kutakuwa na vita kubwa ya mabondia wetu hawa kuwadhihirishia Watanzania namna gani walivyoweza kujiandaa kwa ajili ya pambano hilo,” alisema Salum.
Ikumbukwe mabondia wengine watakaopanda ulingoni kwenye mapambano ya utangulizi yakiwa ni Emmanuel Mwakyembe dhidi ya Francis Miyeyusho, MBaraka Mtange dhidi ya Hamza Mchanjo, Mwinyi Mzengela vs Ajemi Amani, Abdul Kubila vs Msabaha Salum, Omary Baraka vs Muksin Kizota, Ahmady Pelembela vs Idd Pazzy, Adam Mbega vs Oscar Richard na Florah Malechela vs Halima Bandola.
Story na Ibrahim Mussa