Mara nyingi tumezoea mtu unapofanya kazi basi utalipwa, ama unapofanya kazi nzuri utapongezwa lakini haipo hivyo kwa klabu ya soka ya Mtibwa Sugar ambao toka wachukue ubingwa wa Azam Sports Federation Cup mwezi Juni mwaka huu mpaka leo hawajalipwa zawadi yao ya Milioni 50.
Mtibwa Sugar waliifunga Singida United katika mchezo wa fainali ya ASFC pale Jijini Arusha ambapo Kama kawaida walitakiwa kupewa Milioni 50 Kama zawadi ya kuwa Bingwa lakini hadi leo mbali na pongezi za mdomo hawajapewa hata mia ya zawadi yao.
Thobias Kifaru Ligalambwike ambaye ni afisa habari wa Mtibwa Sugar amesema mpaka leo anaisafisha Mfano wa hundi waliyopewa ikiambatana na kombe akisubiri hela zao, lakini ajabu ni kwamba kwenye akaunti yao haijaingia hela yoyote.
“Huwa naingalia hundi tuliyopewa na Mara nyingi huwa naisafisha safisha nikidhani hela itaingia lakini hakuna chochote, sitaki kusema sana naamini TFF watatusikia siku moja na kutupatia hela yetu, naamini ipo sehemu salama,” Kifaru alisikika akihojiwa na Radio Free Africa.
Taarifa zinasema wadhamini ambao ni Azam TV wameshatoa fedha kwa TFF muda mrefu lakini hata TFF wakiulizwa wamebaki kusema kuwa waulizwe Mtibwa Sugar.