Nurdin Hamad Bakari mchezaji wa zamani wa Simba SC anakumbukwa kwa mambo mawili jambo moja ni baya kwenye historia yake na ya Taifa kwa ujumla na jambo jingine ni zuri kwa soka lake binafsi, Nurdin Bakari alikuwa ni sehemu ya ile iliyokuwa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti boys ya MWAKA 2004 ambao walifanikiwa kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, zilizofanyika Gambia mwaka 2005.
Lakini kwa bahati mbaya, Tanzania haikwenda kwenye fainali hizo baada ya kuondolewa na baadae kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Tanzania ilifungiwa kwa sababu timu yake ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ilikutwa na hatia ya kutumia mchezaji aliyezidi umri, na mchezaji huyo alikuwa ni Nurdin Hamad Bakari wakati huoakichezea Simba SC ambayo ilimsajili kama kijana aliyezaliwa mwaka 1983 kwa mashindano ya vilabu vya Afrika mwaka 2003, huku mwaka Mmoja baadae TFF mkimuidhinisha kama kijana aliyezaliwa mwaka 1986 na kumfanya kuwa mchezaji ndani ya iliyokuwa timu ya vijana chini ya miaka 17 Serengeti Boys.
Kumbukumbu pekee nzuri ya Nurdin Bakari ni goli lile lililoepeleka Taifa Stars kwenye fainali za mara ya kwanza za wachezaji wanaocheza ligi za ndani za CHAN, chini ya kocha Marcio Maximo dhidi ya Sudan ya Khartoum, huko Khartoum Sudan.
Leo tukiwa tumebakiza siku therathini tu kumaliza mwaka huu wa 2014, miaka kumi toka ile nafasi ya kipekee tuliyoipata ya kufuzu kwenda Gambia kwa mashindano ya Afrika 2005 hakuna hatua yoyote tuliyopiga katika soka la vijana, na katika kile ninachokiamini dhambi ya Udanganyifu wa Umri wa ile timu yetu ya vijana ya Serengeti Boys ya Mwaka 2004 ni mchezaji Mmoja tu ambae bado anacheza soka katika Ligi kuu yetu ya Tanzania akiwa moja ya vilabu vikubwa ila na yeye ni mchezaji wa Akiba yaani ni mchezaji asiye na namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha klabu yake huyu pekee ni Nizar Khalfani.
Wako wapi akina Athumani Iddi ‘Chuji’, Omar Matuta ‘Wanchope’, Amir Maftah, Juma Jabu, David Mwantobe na wengineo Bahati mbaya kwao, Vijana hao wa wakati huo kwa sasa wanaitwa wazee, swali la msingi kwanini wanaitwa wazee? Kwa hesabu za kujumlisha na kutoa toka mwaka 2004 hadi leo 2014 ni miaka 10 imepita kwa vijana wale ambao walikuwa chini ya miaka 17 na wengine wa miaka 17 kipindi hicho leo hii wana miaka 27 au 26 au chini ya hapo.
Kwa kijana wa miaka wa 26 au 27 umri ambao wataalamu wa masuala ya soka wanasema ndio umri ambao mchezaji anakuwa amepevuka na kuwa mchezaji kamili kwetu sisi imekuwa tofauti, cha kujiuliza nini kimewapata hawa vijana kama sio kudanganya umri? Ninachokiamini katika timu ile kulikuwa na kina Nurdin Bakari wengi sana ambao walikuwa na umri mkubwa wa miaka zaidi ya 17 ila kwa dhambi yetu ya udanganyifu wa umri tukawarudisha zaidi ya miaka 5 hadi 7 yaani kwa kijana aliyekuwa na umri wa miaka 25 kipindi kile au mwenye miaka 23 kipindi kile leo hii ana miaka 33 au 35 hivyo lazima atakuwa nje ya mchezo huu maridhawa wa soka, umri umemtupa nje.
Dhambi ya kudanganya umri ni mbaya sana nakumbuka wakati nakuwa nilizoea kumsikia Athuman Idd Machuppa kwa kwa majina yake hayo, ila nilikuja kushangaa kijana yule akitumia jina la Mohamed Abdallah unajua kisa cha kutumia jina lile la Mohamed Abdallah? Ni dhambi ya udanganyifu wa Umri tu nasikia ile timu yetu ya Taifa ya Ngorongoro baada ya kukosa kupata mshambulizi mahiri tukielekea kucheza na timu ya taifa ya Nigeria kipindi hicho mjanja Mmoja alitoa ushauri wa kumbadirisha jina Athuman Machuppa na hivyo kujulikana kwa jina la Mohamed Abdallah lakini licha ya jitihada hizo bado timu yetu ya chini ya miaka 20 kipindi hicho ilifungwa na kutolewa na vijana wale wa Nigeria.
Dhambi ya kudanganya umri ni hatari sana inamfanya hata yule anayedanganya umri kuamini ule umri aliodanganya ni umriwake na halisi, unalikumbuka sakata la yule aliyekuwa Miss Tanzania pamoja na vielelezo vyote kuwekwa wazi kuanzia leseni ya udereva, kadi yake ya kumruhusu kuishi Marekani, na Pasi yake ya kusafiria kuwekwa hadharini lakini bado aliendelea kuukana umri wake na kutuhakikishia kuwa yeye ana umri wa miaka 23!
Ni wiki kama mbili hivi nilikuwa na kiongozi Mmoja wa klabu moja kubwa nchini nikamuuliza nini maoni yake kuhusu udanganyifu wa umri, alichonijibu ni kwamba hata yeye hajui maana anajitahidi kupambana na udanganyifu wa umri lakini anakosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wenzie, na kuendelea kuniambia kuwa tatizo la watoto wetu hawakui, ukionyeshwa motto mwenye umri wa miaka 17 unawezasema ana miaka kumi na 13 au 14! Na hapa ndipo tunapohalalisha Udanganyifu wa umri.
Ile timu ya vijana chini ya miaka 15 iliyoenda jijini Gaborone Botswana kwa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15, ikaibuka kashfa ya kuwatumia wachezaji watano wenye umri uliovuka na inasadikika kuna wawili walikuwa wana umri wa miaka 20! Hapa tunamdanganya nani kama sio kujidanganya wenyewe? Malengo yetu ni kushinda vikombe na zawadi mbalimbali na sio kuendeleza mchezo huu pendwa.
Sasa imebakia historia imepita miaka 10 sasa toka timu ile iliyojaa vijana waliodanganya umri kwa makusudi mazima ya viongozi wa mpira wa Taifa hili, na Tanzania haijaweza kurudia mafanikio hayo licha ya vizazi tofauti kupita kwa kipindi chote hicho na hii yote ni kutokana na kukosa mipango thabiti na endelevu kubwa likiwa ni kuamini katika udanganyifu wa umri.
Katika kuhakikisha Tanzania inarejesha mafanikio ya Serengeti Boys mwaka 2004, TFF chini ya utawala mpya wa Jamal Emil Malinzi imeomba kuandaa Fainali za vijana U17 mwaka 2019 ninacho kiamini Malinzi pamoja na sekretarieti yake baada ya kupitia kwa kina na kuona kila mwaka tumeshindwa kufuzu kwa kupitia hatua za mtoano njia rahisi ni kuandaa mashindano ya vijana ili tuweze kushiriki.
Swali la msingi hapa uko wapi weledi kwenye jambo hili? Kama hatutakuwa na mipango thabiti ya kutufanya tuwe na timu bora na yenye umri sahihi kushiriki mashindano ya mwaka 2019 kwanini tuandae halafu tutumie wachezaji kwa kudanganya umri?
Katika kufikia lengo lao hilo la mwaka 2019 TFF imeanzisha mfuko maalum wa kusaidia maandalizi ya timu hiyo, ambao utakuwa chini ya rais wa zamani wa shirikisho hilo, Tenga, mfuko huo utasimamia timu mbili za vijana chini ya umri wa miaka 12 itakayoanza kuandaliwa mara moja kwa ajili ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa 17 mwaka 2019 pamoja na U14 ambayo itawania tiketi ya Fainali za U17 mwaka 2017 nchini Madagascar.
Kuanzishwa kwa mfuko huu ni jambo bora na la kulipongeza lakini jambo lililonisina ni mapato ya mfuko huu kuambiwa yatakuwa makato ya asilimia 5 za pesa za udhamini kwenda kwa vilabu, nimekaa peke yangu nikatafakari sana nikashindwa kuelewa kuwa Viongozi tuliowapa dhamana pale TFF wameshindwa kuja na mpango mkakati ambao unaoweza kuwafanya kupata pesa za kuziandaa programu zao hizi mbili.
Mwaka 2004 Shukrani za dhati ziwaendee IPP Media Limited ambao kupitia vyombo vyao vya habari vya kizalendo, ITV na Radio One waliongoza harambee ya kuhamasisha Watanzania kuichangia Serengeti Boys. Watanzania wenye viroba vya ngano, sembe, sarafu, maharage, dagaa, mbuzi, ng’ombe, kuku, noti na chochote walivikusanya studio za ITV na Radio One pale Mikocheni, Dar es Salaam kabla ya kupelekwa TFF viisaidie Serengeti Boys.
Toka mwaka 2004 hadi mwaka huu wa 2014 tukielekea mwishohakuna programu yoyote wala mipango thabiti za kuendeleza soka letu la vijana toka tulipofungiwa mwaka ule wa 2004 kwa kesi ile ya Nurdin Bakari, na hatujui tunafata falsafa ipi katika kuendeleza soka letu la vijana, tumekuwa watu maarufu wa kusoma na kusifia mno miradi endelevu ya wenzetu bila kuchukua hatu za dhati.
Niwakumbushe tena nilishapata kusema huko nyuma TFF haiwezi kumiliki Timu yoyote ile iwe ya vijana ama ya wakubwa, ulikuja ule mradi wa kutafuta wachezaji mitaani na kuwapeleka Tukuyu wilayani Rungwe kwa kambi niliupinga mno kwasababu sikuona kama ile ilikuwa njia sahihi wako wapi wale vijana waliovunwa katika mradi ule? Hakuna hata Mmoja aliyeweza kupata nafasi kwenye vilabu vyetu pendwa wale waliopata usajili, wale wengine nasikia wamerudi makwao baada ya wajanja wachache kuamua kuzipiga zile pesa kwa staili ile ile ya kila siku ya kulipana fadhila baada ya kumfanya Bwana Mkubwa kuwa Raisi pale TFF, nilikuwepo pia uwanja wa Azam Complex pale Chamazi nikiitazama Timu ya vijana ya Serengeti Boys ikicheza na wenzao wa South Africa niliiona timu iliyokosa malengo, watoto ambao hawajafundishwa mbinu za mpira nilimuandikia Kocha wa Timu ile Bwana Hababuu nikimwambia “Hababuu watoto wanafundishwa kucheza mpira na si vinginevyo…….”
Wazungu wana usemi wao mmoja “you can’t teach an old dog new tricks”, Huwezi Mfundisha mbwa mzee mbinu mpya, ndio huu usemi una maana kubwa sana, Serengeti Boys ni kundi la watoto ambao kila mmoja alijiongoza mwenyewe ndani ya uwanja kwasababu tu ana mbinu zake za kuucheza mpira na sio jinsi walivyofundishwa na walimu wao.
Naiangalia Tanzania kwa macho ya mashaka, naiangalia TFF kwa macho ya hasira, naiangalia Wizara ya Michezo kwa macho yaliyojaa chuki, ndio nina Chuki, nina Hasira na nina Mashaka kwasababu sio tu kwenye mpira wa miguu hatufanyi vizuri bali kwenye michezo yote, hatufanyi vizuri na wala hatuna mipango thabiti ya kujikwamua kutoka hapa tulipokwama, tumekuwa mafundi wa kuongea sana kuliko kutenda.
Tumekuwa mafundi wa kudanganya umri mno kuliko kutafuta vijana wa kuwafundisha ABC za mpira, tumebaki kwenye imani kuwa mpira ni kipaji katika karne hii ambayo wenzetu wanaamini mpira ni sayansi ambayo watu wanaingia darasani kusoma na kuja na mikakati thabiti, haishangazi kwa zaidi yamiaka kumi tumekuwa tunawategemea Kelvin Yondani na Nadir Haroub huku hatuwaoni warithi wao wa karibu wala wa baadae.
Nchi za jirani za wenzetu pamoja wamekuwa hawana matokeo mazuri kwenye mashindano tunayoshiriki nao, lakini wamekuwa mstali wa mbele kwenye kuzalisha vipaji vipya kila mwaka, na sisi tumekuwa mafundi wa kupiga hodi kwao kuwasajili kwa pesa nyingi mno na kuacha kuendeleza vijana wetu kwasababu tu tumekuwa washabiki wa njia za mkato kuliko katika mikakati ya muda mrefu.
Vilabu vyetu navyo vimekuwa havina mbele wala nyuma, havina sera ya kulea watoto wala wachezaji wao, wanachokifanya ni kukusanya makundi ya vijana waliodanganya umri na kuwaweka pamoja kwa minajili ya kuwawezesha kushiriki mashindano ya umri yanayoandaliwa na TFF baada ya mashindano kuisha hakuna yanayoendelea hivyo wale vijana kurudi makwao na kukosa muendelezo.
Ifike wakati sasa tuseme hapana, na kusimamia kwenye hapana yetu, ifike wakati tuwaambie viongozi wa vilabu vyetu tunataka kuona maendeleo ya timu zetu ndani na nje ya uwanja, tuone viongozi wakisimamia Soka la Vijana kwa uthabiti kabisa, Washabiki na Wanachama wa Vilabu vya Simba na Yanga wanayonafasi kubwa ya kuleta mabadiliko kwenye vilabu vyao, wawaulize viongozi wao nini wanafanya? Kuwaletea mafanikio na maendeleo na sio kunenepesha mifuko yao kwa pesa za vilabu na kuwafanya waishi maisha ya kifalme huku soka likiendelea kudorora.
Ni wakati muafaka sasa kukabiliana na tatizo hili la Umri, Viongozi wa TFF na Vilabu kwa pamoja tuazimie kuacha kutumia wachezaji waliozidi umri, tuweke mikakati iliyojaa weledi tutumie mashine za kupima umri na si kutumia macho yetu, niwaibie siri tu watu wa Afrika, Asia na Amerika kusini wanaongoza kwa kudanganya umri kwasababu moja kubwa wanachelewa mno kuzeeka kwa muonekano, lakini huwa hawanauwezo wa kupambana viwanjani kwasababu tu Umri wao umewatupa mkono hivyo kupelekea kushukiwa juu ya umri wao, Yuko wapi Haruna Babangida, Obafemi Martins, Michael Essien kwa macho unawaona vijana lakini kwa vitendo vyao uwanjani unagundua dhambi ya kudanganya umri imewatafuna.
Tuache mara moja kujihusisha na udanganyifu wa umri kama kweli tunataka maendeleo ya kweli kwenye Mchezo huu maridhawa wa Soka.
-Eric Zomboko (Dizo Moja)