Ukifuzu kucheza hatua kubwa za mashindano makubwa kama haya ni lazima ukubali kucheza na timu bora kuzidi wewe ambazo zipo ndani ya mashindano husika.
Taifa Stars baada ya kufuzu Afcon mwaka 2019 tumefuzu kwa mara nyingine tena mwaka 2024 na tayari tumefahamu timu ambazo tutacheza nazo ambazo ni Morocco, DR Congo na Zambia.
Tuanze na Morocco ambao walikuwa Poti ya kwanza ambayo walikuwepo vigogo wakubwa pia kama Egypt, Tunisia, Senegal, Algeria na Tunisia! Hakuna asiyejua ubora wa Morocco hii ni “Top Quality” kwenye kundi F kuliko timu yoyote.
Kwenye viwango vya FIFA Morocco wapo nafasi ya 11 ambayo ni juu zaidi ya timu nyingine ambazo zipo ndani ya kundi hilo Tanzania, Zambia na DR Congo! Morocco wamepewa nafasi kubwa ya kufuzu kwenye kundi hili lakini haina maana kwamba hawezi kupoteza dhidi ya hizo timu.
DR Congo! Hawa walikuwa Poti ya pili ambayo pia ilikuwa na timu nyingi zenye ubora mkubwa kama Mali, Ghana, Nigeria na timu nyingine. Sio timu ya kubeza pia sababu ni watu ambao wametuzidi kwenye ushiriki wa michuano hii na viwango vya FIFA wapo nafasi ya 70.
Zambia! Hii ni timu nzuri pia ambayo walikuwa Poti ya tatu na timu kama South Africa, Equatorial Guinea, Mauritania, Guinea na Cape Verde ambao nao wametuacha kidogo wakiwa juu yetu.
Zambia kwenye viwango vya FIFA wapo nafasi ya 86 ambayo ni juu zaidi kulinganisha na sisi pia wana wachezaji wengi sana ambao wanacheza Ligi kubwa Afrika na nje ya bara hili.
Hizi zote ni timu ambazo zimeiacha Tanzania katika hatua ya ushindani kwa kuangalia Poti walizokuwepo kulinganisha na sisi ambao tupo nafasi ya 130 kwenye viwango vya FIFA na jana tulikuwa Poti ya nne pamoja na timu kama Gambia, Namibia.
Kwa uhalisia kwa kundi ni kwamba Tanzania imepangwa na timu ambazo zimechaucha sana kwenye kiwango cha ubora wa ushindani lakini hii haina maana kuwa hatuwezi kushindana ndani ya kundi hili.
Muda wa maandalizi upangwe vizuri kila mtu awajibike kwenye eneo lake ili kwenda kushindana pale mashindano yakianza sababu kundi letu tayari limefahamika.