Nambole, Uwanja mgumu sana kwa kila timu ambayo inakanyaga pale.
Ni ngumu sana kuifunga timu ya taifa ya Uganda katika uwanja huo, kwa sababu pale ndipo sehemu ambayo wachezaji wengi wa Uganda hutoka jasho la damu.
Jasho lao ni tofauti sana na jasho la wachezaji wengi kipindi wanapokuwa Nambole.
Watahakikisha kwa kila tone la damu linalotiririka katika ngozi ya mwili wao kama jasho linalipwa na ushindi ili kuwafurahisha wananchi wa Uganda.
Kitu ambacho wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa sababu Mara ya mwisho kwao kufungwa katika uwanja huo ilikuwa mwaka 1997.
Miaka ishirini na moja iliyopita hawajawahi kuonja uchungu wa kufungwa katika uwanja huo wa Nambole.
Kila shabiki anayekanyaga jukwaa la Nambole huwa na furaha kwa sababu anajua Nambole ni sehemu ya kuzalishia furaha.
Hawajawahi kuwa na wasiwasi! , haijawahi kutokea hata siku moja Waganda wakawa na uoga wakiwa kwenye jukwaa la Nambole hata kama wanacheza na nani.
Ndiyo uwanja ambao Ghana iliyokuwa katika kiwango cha juu ilishindwa kupata matokeo.
Ndiyo uwanja ambao Misri iliyokuwa katika kiwango cha juu ilishindwa kupata ushindi.
Kwa kifupi huu ndiyo uwanja ambao Mohammed Salah alishindwa kufunga goli.
Unajua ni kwanini ? Kwa sababu Uganda walikuwa bora sana.
Uganda walikuwa na timu imara sana mwaka kwa miaka mitatu iliyopita.
Timu ambayo ilitengenezwa katika misingi bora chini ya kocha Micho.
Micho alitengeneza Uganda ambayo ilikuwa inaogofya. Alikuwa na vikosi takribani vitatu vya timu ya taifa.
Vikosi ambavyo vilikuwa na nyota wengi ambao walifaa kucheza katika kikosi cha kwanza!.
Micho aliwekeza muda mrefu kutafuta wachezaji bora ambao wangeweza kucheza katika hali ya kujituma wakiwa na timu ya taifa ya Uganda.
Aliwapata!, akakaa nao, akawalisha sumu ya kupigana , kila mchezaji akawa anajua thamani ya jezi ya timu ya taifa ya Uganda.
Kila ambaye alikuwa anapewa nafasi kuivaa timu ya taifa alipigana kwa ajili ya masilahi mapana ya timu yake ya taifa.
Uganda ikawa timu inayoangaliwa sana, ikawa timu ambayo inatoa ushindani mkubwa ndani ya uwanja.
Ikawa timu ambayo mara mbili mfululizo ikatolewa hatua ya mwishoni kwenye kuwania kufuzu kombe la dunia na michuano ya Afrika (Afcon).
Uganda ikawa timu ambayo ilifanikiwa kufuzu mashindano ya Afrika (Afcon) baada ya kukosa mwishoni mwishoni kwa miaka miwili mfululizo.
Micho aliondoka baada ya mashindano ya Afcon yaliyopita. Hakutaka tena kuendelea kukaa Uganda, Afrika Kusini kukawa makazi yake mapya.
Moses Basena akaaminiwa, akakaa na timu ya taifa kwa muda. Hapo ndipo mwanzo wa timu ya taifa kuporomoka ulipoanza.
Hakuwa na ushawishi mkubwa kama ambao alikuwa nao Micho.
Wachezaji wakawa hawapigani kwa nguvu kama mwanzo ambavyo walikuwa wanapigana.
Moses Basena alikaa kwa muda mfupi, mwezi wa kwanza mwaka huu Mfaransa Desabre alipewa mikoba ya kuiongoza timu ya taifa.
Mfaransa ambaye alikuwa na rekodi nzuri. Rekodi ambayo ilikuwa inawapa imani kubwa Waganda kuwa chini yake watafanya vizuri.
Safari yake ikaanza, safari ambayo ilikuwa ngumu kwa sababu alitakiwa kuendeleza mafanikio ambayo Micho aliyaacha.
Mafanikio ambayo yalitakiwa kutunzwa, mafanikio ambayo Waganda wengi hawakutaka kuyaona yakipotea kirahisi.
Walitamani kufuzu tena katika michuano ya Afcon, walitamani tena kuwa wababe kwa kila mtu ambaye waliyekuwa wanakutana naye.
Lakini chini ya Desabre hadhithi imekuwa tofauti sana, timu yake imekuwa ikihangaika sana kupata matokeo tangu aanze kazi mwezi wa nane.
Mechi tisa (9) alizoiongoza timu ya taifa amefanikiwa kushinda mechi moja tu!.
Kitu ambacho ni kigeni sana kwa Uganda kwa miaka ya hivi karibuni.
Kibaya kinachoumiza mechi ambayo ameshinda, ameshinda dhidi ya kisiwa cha Sao Tome.
Timu ambayo ni dhaifu, ule ubabe wa Uganda umepotea. Ule ushindani wa Uganda umepungua, hata ukatili wa Uganda umetoweka sana na imekuwa Uganda ya kawaida iliyo dhaifu.