Sambaza....

Afcon mara tatu historia nyingine imeandikwa, hongera sana Taifa Stars, asante benchi la ufundi chini ya Adel Amrouche na bendera ya Tanzania imepeperushwa vyema na wachezaji.

Ni 2024 tena baada ya 1980 na 2019 inapendeza sana kwa soka letu, wachezaji wetu na Taifa letu la Tanzania! Timu imeamua kwenda kupambana ili kuandika historia nyingine tena ugenini, sio ugenini tu bali ni pale Algeria.

Sio kila timu itapata matokeo ndani ya Dimba la Stade du 19 Mai 1956 , Algeria! Pale tumewahi kufungwa 7-0 Mwaka 2015 lakini siku ile ilikuwa tofauti sana. Wachezaji walifanya karibu kila kitu kwa usahihi hasa kujilinda kuanzia wakiwa na mpira au bila mpira.

Kibu Denis.

Adel Amrouche aliacha kelele za watu kuhusu uchaguaji wa wachezaji ziendelee halafu yeye akachagua kwenda na Falsafa yake kupitia wachezaji wake ambao amewaita kwa lengo la kuipambania bendera ya Tanzania! Najua wengi mmesahau kumpongeza lakini mimi huyu namuona kama dereva wa Taifa Stars kwenye safari ya jana kuelekea Afcon.

Rangi nne zenye thamani kubwa sana za bendera ya Tanzania zimepepea vyema, bendera ya nchi imesimama na kuweka historia mpya kwenye ardhi ya Mwarabu! Ndio hii nchi yenye mlima mrefu Afrika nzima na ziwa lenye kina kirefu zaidi hapa, tumefika na huu ndio mwanzo.

Sio safari tu bali ilikuwa vita ya soka mbele ya washindani wawili dhidi yetu! Uganda akitaka tufungwe ili afuzu Afcon huku Algeria akihitaji kuweka heshima. Mada kuhusu kupeperusha bendera yetu pale Ivory Coast ndio imeanzia hapa na sisi tunasimama nayo.

Kikosi cha Stars kilichoanza dhidi ya Algeria.

Ile haikiwa Mechi tu ya kawaida bali mechi ya mpira wa miguu dhidi ya mabingwa wa Afcon mara mbili na timu ya pili kwa ubora Barani Afrika ambayo ni Algeria! Sikumbuki ni dakika ya ngapi Djamel Belmadi (kocha wa Algeria) alikaa kwenye kiti ndani ya zile dakika 90 za mchezo pale Algeria.

Unadhani kocha mkuu wa Algeria Djamel Belmadi alipenda kufanya yale mabadiliko ya wachezaji watatu ile Dakika ya 68 ya mchezo? Hapana, lakini Himad Abdelli, Aymen Mahious na Badredini Bouanani waliulizwa maswali mengi sana kwenye ukuta ule wa Taifa Stars usiku ule wa mechi.

Historia nyingine katika Taifa letu, hongereni wachezaji!

 


Sambaza....