Klabu ya Simba leo mbele ya Waandishi wa habari imemtangaza Selemani Matola kuwa kocha mkuu wa timu zake za vijana za Simba akishirikiana na meneja Patrick Rweyemamu katika kitengo hicho.
Simba wakishirikiana na MobAid wameanzisha program inayoitwa “Wakati Ujao” ambapo itatoa fursa kwa timu hiyo kuandaa na kupika vijana ambao watakua na msada mkubwa si tu kwa Simba bali pia kwa nchi kiujumla.
Mtendaji mkuu wa klabu ya Simba Imani Kajula amesema “Ukichunguza timu kubwa za Afrika wana timu za vijana imara ambazo baadae wanaingia kwenye timu ya wakubwa. Leo tunatoa taarifa la kuboresha timu za vijana, la kwanza ni Mkuu wa Programu za Vijana wa Simba, Patrick Rweyemamu,” alisema na kuongeza
“Hakuna mtu bora kumfanya kuwa Kocha Mkuu wa timu za Vijana kama Selemani Matola. Hii inajumuisha timu za vijana za miaka 20 na miaka 17.”
Nae Selemani Matola baada ya kukabidhiwa majukumu hayo ameonekana kufurahia na kuyapokea kutokana na historia yake nzuri katika kitengo hicho aliyoifanya mwaka 2008 mpaka 2012 akiwa na timu za vijana za Simba.
Selemani Matola “Kwanza tupongeze bodi na uongozi kwa kuona hili, kwetu sisi sio jambo geni. Tulishafanya na tulifanikiwa sana. Naamini sasa tutazalisha vitu vizuri zaidi ikiwezekana zaidi ya ile ya mwanzoni. Sitawaangusha wapenzi wa Simba, tafanya wanachotaka mimi nifanye kwenye Youth Development. “
Nae Patrick Rweyemamu meneja wa Simba baada ya kupewa majukumu hayo alisema Mpira hauwezi kuendelea bila kuwa na uwekezaji kwa vijana. Tulishawahi kufanya hii kazi na matunda yake yanajulikana. Kuanzia 2008 hadi 2015 tumetoa wachezaji takribani 250. Hakuna timu za Ligi Kuu hadi madaraja ya chini hayajawahi kukosa wachezaji ambao wamepita kwenye timu ya vijana ya Simba.”
Wadhamini wa programu hiyo ya vijana ya Simba MobAid kwa upande wao wamesema wanashukuru kwa mtendaji mkuu wa Simba kutekeleza yale yote waliyokubaliana wakati wanasaini mkataba huo.
“Kwanza tutoe shukrani kwa uongozi wa Simba kuanza kufanya kile tulichokubaliana. Tumefurahishwa na hii hatua na tunajua timu tunayoshikiana nayo ina malengo gani chanya kwenye mpira wa vijana kwa maslahi ya timu na Taifa.”- Mwakilishi wa MobiAd, Baraka Mwakyelu.