Leo klabu ya Simba imezindua jezi mpya pamoja na kumtambulisha mdhamini mpya ambae ataonekana katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayotarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki hii.
Katika hafla hiyo iliyofanyika leo jioni katika moja ya hoteli mashuhuri Jijini Dar es salaam klabu ya Simba imeendelea kufanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuendelea kutumia nembo ya “Visit Tanzania” ambapo sasa itakua ni mara ya nne kuitumia katika michuano ya Afrika.
Simba kupitia msemaji wake wamethibitisha kuwa wamekubaliana na mdhamini wao mkuu kampuni ya kubashiri ya M-bet kutumia eneo la kifuani la jezi ya Simba ambao kimsingi ndio wenye haki ya eneo hilo.
“Tumepata baraka zote kutoka kwa wadhamini wetu wakuu M-bet ambao ndio wana haki yakukaa mbele kifuani. Sisi sio madalali hatuwezi kuuza eneo mara mbili.
Tupo hapa ili kumtambulisha mdhamini wetu mpya ambae tutakua nae katika Ligi ya Mabingwa kutokana na M-bet kuwa na katazo la kikanuni kutoka CAF,” alisema Ahmed Ally msemaji wa klabu ya Simba.
Nae Mtendaji mkuu wa klabu ya Simba Imani Kajula alisema alisema wao kama Simba wanaiweka nchi mbele na ndio maana wakaamua kufanya kazi na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Imani Kajula “Tanzania ni nchi ya nne kwa vivutio duniani, sasa leo wenye nchi tunaamua kuiweka nchi yetu mbele. Na ndio maana leo tupo na wadhamini wetu wa nguvu kabisa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Nia na lengo la Simba ni kuhakikisha jezi zetu zinatangaza vivutio vya Taifa. Katika Ligi ya Mabingwa kule mechi zote zitakua mubashara na hivyo tutaonekana na itakua rahisi kuitangaza nchi yetu.”
Pia mwakilishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambae ni mjumbe katika Bodi ya Utalii Benard Mratiro alikiwepo kwenye shughuli hiyo na kutia neno kutoka Wizarani kwa niaba ya Katibu mkuu na Waziri wa Maliasili na Utalii.
“Kule nje mtaitangaza nchi ya Tanzania kama ambavyo mlivyojidhatiti nyinyi wenyewe. Yale makubaliano mliyoweka na Katibu mkuu pamoja na Mkurugenzi wizarani yapo vilevile kama yalivyopangwa,” Benard Mtatiro.