Sambaza....

Klabu ya Simba itashuka dimbani siku ya kesho Jumamosi kuelekea mchezo wao wa robo fainali ya kombe la AzamSports dhidi ya Pamba ya Mwanza.

Mchezo huo wa kiporo utapigwa katika dimba la Benjamin Mkapa baada ya kushindwa kufanyika tarehe ya awali iliyopangwa kutokana na ushiriki wa Simba katika michuano ya Kimataifa.

Afisa habari wa klabu ya Simba Ahmed Ally amesema kesho hautakua mchezo mrahisi lakini wao bado wanalitaka kombe lao baada ya kulibeba mwaka jana mkoani Kigoma wakiifunga Yanga sc.

 

Thadeo Lwanga akifunga bao mbele ya walinzi wa Yanga katika fainali ya Kombe la FA Kigoma katika uwanja wa Lake Tanganyika.                                             

“Tunajua kwamba kila mmoja analitazama hili kombe (kombe la FA) kutokana na umuhimu wa kuweza kuwa nalo na ni kombe ambalo lipo mikononi mwetu hivyo tutafanya vizuri kulitetea.” Ahmed Ally alisema na kuongeza

“Pamba moja ya timu zenye uzoefu na wachezaji wazuri hasa ukizingatia kwamba ipo kwenye hatua hii ina maana ni wapinzani wazuri lakini hatuwabezi sisi tunahitaji kombe.”

Kikosi cha Simba kilichoanza katika mchezo wa fainali ya FA dhidi ya Yanga

Ahmed pia hakusita kuwaita uwanjani mashabiki wa Simba ili waje kupata burudani na kuondoka na furaha.

“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuweza kuona namna tutakavyofanya Uwanja wa Mkapa na watafurahi wenyewe,”. Ahmed Ally alimalizia.

Khalid Aucho wa Yanga akimdhibiti Pape Sakho.

Tayari klabu za Azam Fc, Coastal Union na Yanga zimeshakwenda nusu fainali huku akisubiriwa Simba au Pamba kukamilisha idadi ya timu hizo nne.

Endapo Simba itafanikiwa kuibuka mshindi watakwenda kucheza nusu fainali na Yanga katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha.

Sambaza....