Mnyama Simba ameendelea kuunguruma katika Dinba la Benjamin Mkapa kama ilivyo kawaida yake katika michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbele ya Waganda Vipers.
Kama kawaida ni Mwamba wa Lusaka Clatous Chama “Mwamba wa Lusaka” ndie aliepeleka kilio kwa Vipers baada ya kufunga bao safi kabisa katika kipindi cha kwanza mwishoni kabisa na kudhihirisha Simba ni Chama na Chama ni Simba.
Chama alifunga bao hilo baada yakupokea pasi safi kutoka kwa Moses Phiri na kuwahadaa walinzi wa Vipers na kupiga shuti kali la chini lilomshinda mlinda mlango wa Vipers.
Simba watajilaumu wenyewe kwa kutoka na ushindi mwembamba kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga lakini hawakuzitumia. Shuti la Pape Sakho liliokolewa na mlinda mlango wa Vipers kwa ustadi mkubwa kabisa wakati kichwa cha Saidoo kiligonga mtambaa wa panya kipindi cha kwanza.
Hata kipindi cha pili Simba waliendelea kitebgeneza nafasi kadhaa lakini uhodari wa kipa wa Vipers na kukosa kwa umakini kwa Saidoo kuliwanyima magoli Simba.
Vipers nao walirudi kwa kasi kipindi cha pili na kupelekea kutengeneza nafasi kadhaa lakini uimara wa Aishi Manula uliwaweka Simba mchezoni haswa kisigino cha dakika ya mwisho kilichopigwa na mchezaji wa Vipers.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo Horoya wamekubali kichapo cha mabao matatu kwa moja kutoka kwa Raja Casablanca. Kwa matokeo hayo sasa Simba wamesogea mpaka nafasi ya pili wakiwa na alama sita nyuma ya wababe Raja wenye alama kumi na mbili.
Kwa matokeo hayo sasa ni wazi Simba wana nafasi yakusonga mbele kwani mchezo ujao watakua nyumbani dhidi ya Horoya na ushindi dhidi yao ni wazi watavuka katika kundi wao na Raja Casablanca.