Sambaza....

Mabingwa wa soka nchini Simba Sports Club wameanza vibaya mchezo wa raundi ya kwanza wa ligi ya mabingwa Afrika baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nkana ya Zambia mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Nkana mjini Kitwe.

Simba ambayo iliyoingia kwa kujiamini hasa baada ya raundi ya awali kuwaondoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa jumla ya mabao 8-1 walionekana wachovu huku wakishindwa kabisa kuhimili kasi ya mchezo hasa katika kipindi cha kwanza.

Bao la kwanza la Nkana ambayo anachezea mtanzania Hassan Ramadhan ‘Kessy’ lilipatikana katika dakika ya 27 kupitia kwa Ronald Kampamba kwa shuti kali nje kidogo ya 18 ambalo lilimshinda kipa Aish Manula na kujaa wavuni.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Nkana walikuwa mbele kwa bao hilo, lakini kipindi cha pili Simba waliingia tofauti kuliko kipindi cha kwanza lakini kwa mara nyingine wakaruhusu bao la pili ambalo lilifungwa na Kelvin Kampamba.

Bao hilo liliamsha ari kwa Simba na kuanza kulisakama lango la Nkana hali iliyompelekea beki Musa Mohamed kufanya makosa kwa kumkwatua Meddie Kegere kwenye 18 na mwamuzi kutoka Nigeria Salisu Basheer kuamuru ipigwe penati iliyopigwa kiufundi na John Bocco na kuiandikia Simba bao la kufutia machozi na pengine bao muhimu katika mchezo huo.

Kwa matokeo hayo Simba watahitaji ushindi wabao 1-0 au zaidi katika mchezo wa marudiano utakaofanyika jijini Dar es Salaam kwenye uwanja mkubwa wa Taifa Juma moja lijalo.

Aidha wawakilishi wengine wa Tanzania, Mtibwa Sugar wao wamekubali kichapo kizito cha mabao 3-0 kutoka kwa KCCA ya Uganda kwenye mchezo wa kombe la shirikisho Afrika uliofanyika nchini Uganda.

Mabao yote ya KCCA katika mchezo huo yamepatikana katika kipindi cha pili kupitia kwa Kyambadde Allan, Kadu Patrick na Okello Allan na kufanya Mtibwa kuwa na mlima mrefu wa kupanda katika mchezo wa marudiano kwani itawalazimu kushinda zaidi ya mabao 4-0 ili kusonga mbele hatua inayofuata.

Sambaza....