Sambaza....

Miongoni mwa mechi ambazo haziji kusahaulika barani ulaya na duniani kwa ujumla ni mechi ya raundi ya 16 bora klabu bingwa barani ulaya iliyochezwa Machi 8, mwaka 2017 kati ya Barcelona na Paris-Saint Germain. Ilikuwa ni mechi ya marudiano baada ya ile ya kwanza iliyochezwa pale ufaransa na PSG kuibuka na ushindi wa magoli 4-0, katika mchezo huo wa marudiano pale Nou Camp Barca waliibuka na kitita cha magoli 6-1, na kuwasukuma nje ya mashindano PSG.

Mchezo huo ndio ulioandika rekodi ya kuwa mechi yenye “come back” ya maana katika historia ya mashindano ya klabu bingwa barani ulaya, kwani wengi walitarajia Barcelona wangetolewa baada ya mchezo wa kwanza.

Ukiachana na mechi hiyo, mechi nyingine ni ile iliyochezwa Aprili 4 mwaka huu, katika mchezo wa kwanza wa robo fainali, kati ya Barcelona na AS Roma, Roma ililala Nou Camp kwa magoli 4-1. Katika mchezo huo Barcelona walimiliki mpira kwa asilimia 59 dhidi ya 41 za AS Roma. Katika mchezo wa marudiano pale Stadio Olimpico, Barcelona ililala kwa mabao 3-0, huku wakiachiwa umiliki wa mpira. Barca walimiliki mpira kwa asilimia 57 dhidi ya 43 za AS Roma. Wengi pia hawakuamini kilichomkuta Barcelona baada ya mchezo huo uliopigwa Aprili 10 mwaka huu.

Jiulize kitu kimoja, hivi wachezaji waliikuwa na siri gani ya kuwafanya warudishe magoli yote na kuongeza mengine na kufuzu hatua inayofuata? PSG walitoka huku wakiendelea kumlaumu mwamuzi wa mechi ile. Siri ni moja tu, nayo ni saikolojia ya wachezaji, namaanisha maandalizi ya wachezaji kimwili, kiakili na mtazamo, na hapa ndipo tutaona umuhimu wa kuwa na watu mbalimbali katika timu hasa wanasaikolojia wa michezo.

Simba SC mwishoni mwa wiki hii watakuwa na kibarua kizito mbele ya Nkana Red Devils ya Zambia katika mchezo wa raundi ya pili, klabu bingwa Barani Afrika. Baada ya Simba kukubali kichapo cha 2-1 ugenini, itahitaji kupata goli moja nyumbani ili isonge mbele katika hatua ya makundi.

Goli moja ni rahisi kulitamka na ni gumu sana kulipata, au linaweza likapatikana lakini ikawa ni vigumu kulilinda lisirudishwe. Kwa kikosi cha Simba jinsi kilivyo, na kwa kuitazama Nkana ya mchezo wa kwanza, naweza kusema kuwa beki ya Simba ndio itakayokuwa mwamuzi wa mechi hiyo. Simba iko vizuri katika maeneo mengi lakini katika eneo ambalo lina ubovu mkubwa ni eneo la beki.

Nikianza na golikipa kama sehemu ya ulinzi. Golikipa Aishi Manula  anaonekana kuwa vizuri akiwa golini japo uzuri wake unaweza ukafifia kutokana na changamoto hasa za uchovu, ni  ukweli kuwa, Manula anaonekana amechoka, amecheza mechi nyingi kwa muda mfupi. Goli la kwanza walilofungwa  na Nkana alishindwa kwenda kuhakikisha mpira unakoenda. Wengi walitarajia Manula angesafiri na kuuokoa mpira.

Katika mechi ya Simba dhidi ya KMC, Manula alipumzishwa bila shaka Patrick Aussem alijua fika Manula ana uchovu na anahitaji kupumzishwa. Udhaifu mwingine ambao aliuonesha golikipa huyo ni kutoongea na mabeki wake, jinsi ya kukaa na kuwaamlisha. Unajua golikipa ndiye mchezaji pekee anayeuona uwanja wote, pia anajua mikimbio ya mabeki wake wakati wa kuziba mianya na kukaba, nilitarajia kumuona Manula akiwafokea akina Paschal Wawa, Nicolus Gyan, Mohammed Hussein na Erasto Nyoni lakini Manula aliendelea kuwa kimya, matokeo yake ni kufungwa na nafasi nyingi zikitengenezwa na Nkana.

Kiujumla Simba hawakuwa vizuri katika maeneo yote ya timu katika mchezo wa kwanza ukilimganisha na wenyeji wao Nkana Fc ambao walionekana kuwa na kasi inayohitajika wakiwa katika nusu ya Mpinzani na kuwalazimisha mabeki kufanya makosa na hatimaye kuzawadiwa magoli mawili.

Wachezaji wa Simba wanatakiwa kuandaliwa kisaikolojia. Na Saikolojia kubwa zaidi ni kuwa na  akili ya ushindi “ Winning Mentality” akili zao zikae zikijua kuwa timu inahitaji kufuzu, inahitaji magoli zaidi ya moja, inahitaji kusonga mbele na inahitaji kucheza vizuri na kushinda. Ili kutengeneza huo ushindi wachezaji wa Simba wanahitaji vitu vinne ambavyo ni hivi;

Kujiamini. Naamini kama Simba watajiamini wanaweza kupata goli zaidi ya moja na hatimaye kufuzu kwa kishindo. Ndiyo maana wanahitajika kujengwa kisaikolojia na watu wenye taaluma hiyo kwa kuwa kuna athari moja inaweza ikajitokeza nayo ni kujiamini kupita kiasi. Wachezaji inatakiwa wajiamini , waamini kuwa wanaweza kuwanyamazisha Nkana.

Ari ya mchezo. Hizi ni hamasa ndani ya mchezaji mmoja  mmoja, ndani ya moyo wake. Binadamu ili afanye kitu kiusahihi anahitaji kufanya juhudi, na juhudi hutokana na hamasa ndani ya mtu mwenyewe, Vivyohivyo wachezaji wa Simba wanahitaji hamasa kutoka ndani ya mioyo yao “Intrinsic Motivation”. Kama watafanikiwa kujiahamasisha wenyewe basi wanaweza wakawa wepesi kuhamasishwa.

Kuwa mchezoni. Wachezaji kwa sasa inatakiwa wawe mchezoni. Maandalizi ya mchezo huchukua siku nyingi, lazima wachezaji wawe tayari kiasi cha kuona siku zinachelewa. Kama watakuwa mchezoni kwa siku zote bila kukutana na masuala yatakayowaweka nje ya mchezo tutarajie Simba kufanya vizuri. “Concentration and focus” ndicho kitu kinachohitajika nje na ndani ya uwanja, na hatimaye kushinda mechi. Hizi mechi zina vitu vingi lakini uzuri hii sio Simba na Yanga bali ni Simba na Nkana, hivyo naamini wachezaji wataandaliwa kiushindi zaidi.

Kufanya vizuri kwenye presha kubwa. Hii ni saikolojia bhana! Haiji kutoka mbinguni bali ni maandalizi ya kitaaluma kwa mchezaji ili afanye vizuri katika mchezo. Ni wachezaji wachache wenye uwezo wa kuonyeha vipaji vyao kwenye mechi kubwa, na hii ni kuzidiwa uwezo na presha ya mechi. Wachezaji wa Simba lazima waandaliwe katika hali ya kupambana na kucheza kwa ari kukiwa na shinikizo, presha na vigingi vingi. Kwa kimombo unaweza kusema “ Composure under pressure” bila hiki kitu Simba italala  taifa.

Wastani wa umri wa wachezaji wa Simba ni miaka 25, huku kikosi cha kwanza kikiwa na watu wenye uzoefu mkubwa na mashindano haya na hata na mataifa yao akiwemo Meddie Kagere, Okwi, Boko na Manula. Kama wachezaji hawa wenye uzoefu wataongea na kutoa ushawishi kwa wengine na kwenda kwa ajili ya kupambana basi Simba huenda ikapiga hatua.

Na kama Simba haina mwalimu wa Saikolojia (Mental Game Coach) bila shaka Kocha mkuu inabidi awe muhamasishaji mkuu wa kikosi chake, kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa na ari ya kupambana kimbinu, kimkakati, kinguvu na kiakili kuhakikisha Simba inasonga mbele.

Wachezaji wa Simba kwa sasa hawahitajiki kujifua mwili, na mazoezi pekee, pia hata akili zao (Saikolojia) lazima iwekwe sawa kwa wachezaji. Wachezaji wakiwa na saikolojia nzuri kisha wakafanya mazoezi na kusawazisha makosa katika maeneo yote ya timu, kutokana na hitaji la mechi, Simba inaweza kushinda lakini kinyume na hapo ni “hamna kitu”.

Sambaza....