Wekundu wa Msimbazi Simba wametua salama nchini Morocco wakiwa na kikosi kamili tayari kabisa kuelekea katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Raja Casablanca utakaopigwa katika uwanja wa Mohamed wa VI.
Tayari wachezaji wote wa Simba wameshafika nchini Morocco, wale waliokua na timu zao za Taifa wameshawasili nchini humo kuungana na kundi la kwanza waliotangulia tangu awali.
“Kikosi kimewasili nchini Morocco saa tatu asubuhi ambapo huku kwetu ni saa sita mchana huku wachezaji wakiwa kwenye hali nzuri.
Wachezaji wanne waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Aishi Manula, Beno Kakolanya, Mzamiru Yassin na Shomari Kapombe ambao waliondoka nchini jana mchana walikutana na kikosi Qatar na kuunganisha pamoja mpaka Morocco,” taarifa rasmi ya klabu ya Simba ilisema.
Simba wanakwenda Morocco kwenda kukamilisha ratiba kwani tayari wao na Raja Casablanca wameshafuzu kwenda robo fainali na Raja yupo kileleni wakati Simba ni wapili ambapo hata wakishinda hawabadili msimamo.
Kuelekea mchezo huo Simba itamkosa Mohamed Hussein Tshabalala mwenye kadi mbili za njano pamoja na Kibu Denis. Simba pia wanapaswa wawe makini na machagua ya kikosi chao kwa kuna wachezaji muhimu wameshaonyeshwa kadi ya njano hiyo wakipata kadi katika mchezo huo wataukosa mchezo wa kwanza wa robo fainali.
Baadhi ya nyota wenye kadi moja ya njano ni pamoja na Henock Inonga, Joash Onyango, Moses Phiri na Sadio Kanoute. Ni wazi mwalimu wa Simba atakwenda na machaguo mapya kama Kenedy Juma, Gadiel Michael na Peter Banda ambao hawapati nafasi ya mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.
Kuelekea mchezo huo pia ni vyema Simba wakaanza mapema maandalizi ya jinsi ya kucheza mchezo wa robo fainali wakiwa ugenini kwani timu kariba ya Raja Casablanca ni dhahiri inaweza kuonyesha ni kwa kiasi gani kikosi cha Simba kina mapungufu ama kimetimia katika maeneo gani haswa wakiwa nyumbani.
Mchezo huo kati ya Raja Casablanca na Simba utapigwa siku ya Jumamosi saa saba usiku kwa saa za Afrika Mashariki.