Sambaza....

Azam FC wametolewa katika mashindano ya kimataifa. Inahuzunisha timu iliyosajili vyema, iliyopata muda wa Camp pale Tunisia, kisha inatolewa kirahisi namna ile. Inasikitisha sana.

Binafsi naamini Azam FC wana shida nyingi. Ziko nyingi mno, lakini shida yao kubwa ni mashabiki. Hii ndiyo shida yao kimsingi, kabla hatujatazama shida nyingine.

 

Mashabiki wana maana kubwa katika timu ya mpira. Wanawaweka kikaangoni wachezaji mambo yakiwa hayaendi.

Wanawasukuma wachezaji kuipambania timu. Wanawashangilia wakifanya vyema. Kwa Azam FC hali ni tofauti.

Sio kama Simba SC na Yanga SC hazifungwi katika haya mashindano, lakini unaona jinsi wachezaji wao wanavyopambana. Ule upambanaji unaouna kiwanjani unanzia jukwaani wanakokaa mashabiki.

Mashabiki wa klabu ya Simba katika mchezo wa Kimataifa

Ni ngumu kujua kama Azam FC imeshinda mechi au imepoteza. Hakuna tofauti. Mchezaji wa Azam FC yuko huru katika vitu vingi. Hakutani na wakati mgumu timu inapofungwa. Simba SC na Yanga SC maisha ni tofauti hali ikiwa kama ile.

Kama ingekuwa Simba SC au Yanga SC ndiyo wamefungwa juzi pale Chamazi mpaka kufikia sasa tungesikia taarifa tofauti kutoka kwao.

Tungesikia kiongozi fulani na mchezaji fulani wameshindwa kutimiza majukumu yao. Haya ndiyo maisha ya Simba SC na Yanga SC.

Mashabiki wa Wananchi Yanga.

Mashabiki wanatengeneza presha kwa uongozi na wachezaji, Azam FC hawana watu hawa. Juzi wamefungwa usiku, jana asubuhi wameamkia zao mazoezini. Na fresh tu.

Simba SC na Yanga SC zikipoteza mechi katika namna ile ni kama vile pale Msimbazi au Jangwani kumetokea msiba.

Presha yote hii inatokea kwa mashabiki. Wachezaji hujihisi wana deni la kulipa wakiona uwanja umejaa kwa ajili yao.

Feisal Salum akipiga kichwa mbele ya wachezaji wa timu pinzani.

Wachezaji wale wale wa Azam FC ukiwapeleka Simba SC au Yanga SC wanakupa kitu bora kiwanjani. Watapambana mpaka watapambana tena.

Kuna tofauti ya kuwa mchezaji wa Azam FC, kisha kuwa mchezaji wa Simba SC na Yanga. Azam FC imeziacha Simba SC Yanga SC katika baadhi ya vitu.

Lakini wao wamezidiwa mashabiki, lakini walipaswa kutumia nguvu waliyonayo kukaa katikati ya Simba SC na Yanga SC.

Lakini kinachotokea sasa ni kama vile Azam FC nao ni timu iliyozidiwa kila kitu na haina kitu ilichozizidi Simba na Yanga SC.

Sambaza....