Sambaza....

MLINDA mlango wa Mtibwa Sugar FC, Shaaban Kado amesema kikosi chao kinaweza kufika mbali zaidi katika michuano ya Caf Confederations Cup msimu huu. Mtibwa iliichapa 4-0 Northern Dynamo ya Shelisheli katika mchezo wa hatua ya awali kuwania kufuzu kwa hatua ya makundi jijini Dar es Salaam Jumanne iliyopita.

Mabingwa hao watetezi wa michuano ya FA wataenda kulinda ushindi wao huo Disemba 4 huko ugenini na Kado anaamini wanaweza kusonga mbele. “ Naamini tumeanza vizuri michuano, lakini kazi bado ngumu sana. Tunatakiwa kuendelea kupambana ili kusonga mbele.” Anasema nyanda huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania nilipofanya naye mahojiano mafupi Ijumaa hii.

Shaban Kado

“ Naamini tunaweza kufika mbali sana kwa uwezo wa Mungu na kujituma kwetu. Tuna kikosi bora na chenye vipaji vya kuweza kutusaidia kusonga mbali zaidi katika michuano hii.” Mtibwa inashika nafasi ya nne katika msimamo baada ya kucheza michezo 14.na kukusanya alama 14, na wamepitwa kwa pointi 11 na viongozi wa ligi-Yanga SC.

“ Ligi inaendelea vizuri, timu nyingi naona zipo sawa hata zile zinazoonekana mdogo, msimu huu wamesajili vizuri hali inayoleta ushindani lakini tatizo kubwa lipo katika ukosefu wa udhamini tu, hapo ndiyo kuna changamoto.” Anaongeza kusema golikipa huyo wa zamani wa Yanga ambaye tangu atoke katika majeraha amefanikiwa kucheza michezo isiyopungua 12.

“Kuna vipaji vingi vya kuvutia, hilo ndilo jambo jipya katika ligi ya msimu huu upande wangu. Kama wachezaji watajitambua nafikiri tutakuwa na ligi bora zaidi msimu huu.”

Sambaza....