Klabu ya soka ya Zenit St. Petersburg imemtangaza Sergei Semak kuwa kucha mkuu wa klabu hiyo kuchukua nafasi ya Roberto Mancini ambaye ameondoka klabu hapo na kujiunga na timu ya Taifa ya Italia.
Semak ambaye kipindi akitandaza kabumbu alikuwa akicheza eneo la kiungo, aliichezea Zenit na kustaafu akiwa hapo mwaka 2013 na kuwa kocha msaidizi kabla ya kuwa kocha wa timu ya Taifa ya Russia baadae.
Anajiunga Zenit akitokea FC Ufa ambayo imemaliza ligi ya kuu nchini Russia katika nafasi ya sita ikiwa ni nafasi bora zaidi ambayo klabu hiyo imeipata ikishiriki ligi hiyo na anajiunga na Zenit ambayo yenyewe ilimaliza katika nafasi ya tano.
Msimu uliopita klabu ya Zenit ilitumia kiasi kikubwa cha pesa katika usajili, wakiwasajili wachezaji watano wa kutoka Argentina akiwemo Leandro Paredes lakini wameshindwa kupata nafasi ya kushiriki michuano ya ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 42, ni kipenzi cha watu wa wa Russia na alikuwa kocha pekee mzawa kwa siku za hivi karibuni ambaye aliifundisha timu ya Taifa ukimuondoa Anatoly Davydov aliyedumu miezi miwili pekee kipindi cha mwaka 2009, amepewa kandarasi ya miaka miwili.