Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF rasmi limetoa ratiba ya michezo ya Ngao ya Jamii ambapo kwa mara ya kwanza nchini litashirikisha timu nne ambapo zitafanyika mkoani Tanga.
Timu nne zitakazoshiriki michezo hiyo ni Yanga, Simba, Azam na Singida Fountaine Gate na michezo hiyo itaanza kupigwa August 9 mpaka August 13 mwaka huu Tanga na kuukaribisha mtindo mpya wa michezo ya Ngao ya Jamii.
Mshindi wa mechi hizo atacheza fainali August 13 saa moja usiku wakati wale watakaofungwa watacheza kumtafuta mshindi wa tatu siku hiyohiyo saa tisa alasiri hapohapo Mkwakwani
Michezo ya Ngao ya jamii huchezwa kwa kumaanisha kuukaribisha msimu mpya wa Ligi na hivyo ni wazi bodi ya ligi wapo mbioni kutoa ratiba ya Ligi ambapo mchezo wakwanza wa ufunguzi huenda ukaanza August 15.
Simba na Yanga zimekua na utaratibu wa kutumia Simba Day na Siku ya Mwananchi kutambulisha rasmi jezi, wachezaji na benchi la ufundi kwa mashabiki na wapenzi wao ambapo shughuli hizo hufanyika mwanzoni mwa msimu haswa wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi wa nane.
Simba imekua ikitumia siku ya Sikuu ya wakulima nanenane kama siku maalum ya tamasha lao hilo na hata Yanga pia wamekua wakitumia tarehe sita kama siku yao maalum ya Tamasha hilo hivyo kwa tarehe hizo ni wazi vigogo hao itawapasa kujipanga upya.
Katika ratiba hiyo ya TFF mchezo wa kwanza utaanza kupigwa August tisa mwaka huu ambapo Yanga watamenyana na Azam Fc, wakati August kumi Simba watakua uwanjani dhidi ya Singida Fountaine Gate Fc.
Ili kuwavutia wapenzi, mashabiki na wanachama wake Simba na Yanga huwa zinapanga siku ambayo michuano yoyote inakua haijaanza ili kuwatambulisha mastaa wao kwa mara ya kwanza kabisa katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kufuatia ratiba hiyo ya michezo hiyo ni wazi sasa wakubwa hao watakua wanakuna vichwa ni vipi wataweza kuendana na ratiba hiyo ya Shirikisho la soka nchini ili pia kuendeleza utamaduni wao na kuwapa burudani mashabiki wao.
Si tu Simba na Yanga lakini pia hata Azam Fc na Singida Fountaine Gate nao wamekua na huo utaratibu kwani mwaka jana SFG iliyokua ikiitwa Singida Big Stars na Azam Fc nao walikua na siku kama hiyo huku wakicheza mchezo wa Kimataifa wakirafiki.