Leo fainali sportpesa inafanyika katika mji wa Nakuru ambapo itazikutanisha timu mbili moja kutoka Kenya ( Gor Mahia ) na nyingine ni kutoka Tanzania ( Simba). Zifuatazo ni sababu ambazo zinanipa imani kuwa Simba atapoteza mchezo wa leo.
1: Faida ya Uenyeji kwa Gor Mahia.
Gor Mahia itakuwa katika uwanja wa nchi yake, hivo itakuwa faida kwake kwa sababu ya kuzoea uwanja pia hata hali ya hewa ya uwanjani itakuwa na faida kwake kwa sababu atakuwa na faida kubwa ya kuwa na mashabiki ambao watakuwa wanampa nguvu ya kushangiliwa kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mchezo.
2: Safu bora ya ushambuliaji na ya Ulinzi ya Gor Mahia.
Mpaka sasa Gor Mahia haijafungwa goli lolote na imefunga magoli matano katika mechi mbili walizocheza ambapo waliifunga JKU goli 3-0 na wakaifunga Singida United goli 2-0 hii inaonesha ni timu imara kwenye safu ya ulinzi na kwenye safu ya ushambuliaji ndiyo maana mechi zao hazijafika mpaka katika mikwaju ya penalties tofauti na wapinzani wao Simba.
3: Kukosekana kwa muunganiko wa timu ya Simba.
Simba imepeleka asilimia kubwa wachezaji ambao hawakutumika sana katika ligi kuu na kibaya zaidi imepeleka wachezaji wapya hasa hasa eneo la mbele, eneo ambalo lilikuwa lina John Bocco na Emmanuel Okwi katika michuano ya ligi kuu ambapo walifanikiwa kufunga magoli zaidi ya 30, hii imekuwa tofauti na kwenye mechi za michuano hii ya Sportpesa ambapo timu imekosa muunganiko mzuri katika eneo la mbele kutokana na kutumia wachezaji wengi wapya ambao wanaonekana hawajazoeana na kuizoea Simba.
4: Timu iliyo kwenye mashindano dhidi ya timu isiyo kwenye mashindano.
Gor Mahia iko kwenye ligi kuu ambayo inaendelea tofauti na Simba ambayo imemaliza ligi kuu na wachezaji wake walikuwa wamepumzika tofauti na wachezaji wa Gor Mahia ambao wanekutwa na michuano hii ya Sportpesa wakiwa tayari wanafomu nzuri kutokana na kuwa kwenye ligi tofauti na Simba ambayo imeanza kutafuta fomu kutokana na kwamba wameenda kwenye michuano hii wakitoka mapumzikoni.
5: Aina ya uwanja dhidi ya aina ya wachezaji wa timu zote.
Moja ya tatizo kubwa linalolalamikiwa sana ni uwanja unaotumika katika michuano hii ya sports pesa, ni uwanja usio katika hali nzuri hasa hasa kwenye eneo la kuchezea ( pitch). Eneo hili linawasumbua sana Simba kutokana na utamaduni wa mpira wao ambapo hucheza kwa pasi fupi fupi, uwanja hauruhusu kupiga pasi hii ni tofauti na kwa Gor Mahia ambao timu yao ina uwezo wa kucheza mipira mirefu ambao inaendana na aina ya uwanja huo.