Klabu ya soka ya Gor Mahia ya nchini Kenya imethibitisha Usiku wa kuamkia leo, kupokea barua ya kujiuzulu kwa kocha mkuu Dylan Kerr aliyedumu katika Klabu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Mwenyekiti wa klabu ya Gor Mahia Ambrose Rachier amethibitisha taarifa hizo katika tovuti ya klabu kwa kusema kuwa kocha huyo ambaye alibakisha mwaka mmoja katika mkataba wake amejiuzulu na kutaja kuwa anakwenda katika majukumu mengine.
“Nimepokea barua ya kujiuzulu ya kocha Kerr, kwa niaba ya klabu nathibitisha kuridhia maombi yake kwani amekuwa mtu mwema, na kwa mujibu wa barua yake ametaja kwamba anakwenda sehemu nzuri zaidi, nami namtakia kheri katika majukumu mapya,” Rachier ameuambia mtandao wa klabu.
Katika barua ya Kerr, amewashukuru viongozi wote wa klabu, wachezaji na mashabiki na kusema kuwa angependa kuanza msimu mpya akiwa na timu nyingine.
“Kwa masikitiko makubwa, nimekubali majukumu mengine ya ukocha kwa msimu ujao, napenda kuwashukuru viongozi hasa Mwenyekiti wa klabu kwa kunipa nafasi ya kufanya kazi na nyie na zaidi kwa ajili ya Gor Mahia, kwa wachezaji, nachoweza kusema ni asanteni kwa kuwa wenye kujituma, kila mchezaji amefanya kwa nafasi yake kwa furaha, ufanisi na kujituma, naamini mtaendelea kuwa na maono hayo,” sehemu ya Barua ya Kerr imesomeka.
Aidha Mwenyekiti wa klabu hiyo amewaomba mashabiki Kuwa watulivu wakati ambapo wanakwenda kuchagua kocha mwingine ambaye ataiongoza Gor katika mechi zijazo za Klabu bingwa Afrika ambapo amelitaja benchi la ufundi lililoachwa na kocha Kerr kuendelea na Majukumu yake katika kuianda timu kuelekea michuano ya Afrika.
“Tunajua wote kuwa tunamechi muhimu mwishoni mwa mwezi huu ya Klabu Bingwa Afrika, hakutakuwa na haraka kutafuta mbadala, tutaendelea na benchi la ufundi la sasa, tukijipanga kupata kocha mwingine bora zaidi,” amesema.
Kerr ambaye ni kocha wa zamani wa Simba Sports Club alijiunga na Gor Mahia mwaka 2017 na kusaini mkataba wa miaka mitatu, akiisaidia timu hiyo kushinda mataji mawili ya ligi na kucheza hatua ya makundi kwenye michuano ya kombe la Shirikisho Afrika.