Sambaza....

Baada yakutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu huu kwa kufikisha alama 74 kufuatia ushindi wa katika mchezo dhidi ya Dodoma Rais wa Klabu ya Yanga Injinia Hersi Said ametoa ya moyoni mwake.

Kupitia ukurasa wake wa instagram Hersi Said amesema “Nianze kwa kumshukuru Mola wangu muweza wa yote. Niendelee kwa kuishukuru familia yangu kwa mapenzi ya dhati yasiyo na kikomo yanayonipa kila sababu ya kuendelea kufurahia maisha”

Hersi hakusita kuwashukuru wadhamini wa klabu yake pamoja na wanachama wa klabu ya Yanga akiamini wao ndio sababu kubwa yakupelekea mafanikio hayo na kuwa klabu bora zaidi katika ukanda huu.

“Aidha, kwa muktadha mpana wa klabu yangu pendwa, Klabu Kongwe, iliyofanikiwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, sina budi kuwashukuru kila mmoja kwa nafasi yake,” alisema na kuongeza

“Tuwashukuru sana wadhamini wetu kwakuwa wamekuwa mhimili mkubwa wa ustawi wa kiuchumi wa klabu yetu. Tufahamu pia mchango wa wanachama na mashabiki wetu umekuwa mkubwa sana baada ya klabu yetu kupitia mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji      (TRANSFORMATION)

Ada za uanachama, ununuzi wa bidhaa zenye nembo ya klabu, ununuzi wa tiketi za mechi zetu na ushiriki wa program mbalimbali za klabu umeingiza kipato kikubwa ambacho kimesaidia kutatua changamoto kadhaa za uendeshaji wa klabu yetu.”

Rais wa Yanga Hersi Said (kulia) akiwa na Makamo wa Rais Arafat Hajji.

Pia Injinia Hersi ameonyesha kuheshimu na kuwashukuru viongozi wenzake klabuni hapo kutokana na kazi nzuri na yakutukuka waliyoifanya katika idara zao.

“Kwenu uongozi wa klabu, mmekuwa imara kila kukicha na kupaisha ubora wa utendaji wenu kwenye kila idara. Ninavutiwa sana utendaji wa CEO, kaka yangu Andre Mtine hakika wewe ni mtu bingwa kabisa tena mwenye kustahili Maua yako!

Nisipowataja vijana mnaoshikilia idara nyeti kwa ufanisi mkubwa nitakuwa sijatenda haki! Patrick Simon, CPA Haji Mfikirwa, Alli Kamwe, Priva Shayo, Alwatan Abdulaziz na Anderson Amani. Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wamekuwa chachu ya mafanikio haya. Kipekee kabisa, mchango mkubwa wa makamu wangu Arafat Hajji.”

Hersi pia amewamwagia sifa wachezaji wa Yanga chini ya nahodha wao pamoja na benchi zima la ufundi kwa kufanikisha ubingwa wa Ligi msimu huu.

“Pia, benchi letu la ufundi limekuwa na maingizo mapya machache yenye tija. Kuongezwa hivi karibuni kwa mtaalam wa kusoma mchezo na wapinzani Khalil kumeleta mapinduzi makubwa katika kuendea wapinzani kwa tahadhari na mpango kazi yenye kuleta matokeo chanya.

Kwenu wanajeshi wetu chini ya nahodha wa Wananchi Bakari Mwamnyeto niseme tu mmetuheshimisha sana! Jasho na damu mmelimwaga kupigania furaha ya mamilioni ya Wananchi nasi tunatamba mtaani. Ubora wenu, jitihada zenu, nidhamu yenu, umoja wenu na shauku ya kuendelea kuwa bora zaidi kwa pamoja vimewafikisha hapa kuwa Mabingwa wa NBC Premier League 2022/23,” alimalizia rais wa Yanga Hersi Said.

Sambaza....