Sambaza....

Kikosi cha Yanga tayari kipo nchini Afrika Kusini kuelekea mchezo wa marudiano wa nusu fainali dhidi ya Marumo Gallants baada ya ushindi wa mabao mawili kwa bila walioupata nyumbani.

Wakiwa nchini humo Rais wa Klabu ya Yanga Injinia Hersi Said amesema wanatazamia kushinda makombe yote yaliyopo mbele yao huku wakiwa tayari wametwaa taji la Ligi Kuu ya NBC.

Mpaka sasa Yanga ipo kwenye nusu fainali za kombe la FA na Shirikisho Afrika na akizungumzia siri ya mafanikio hayo akifanya mahojiano na mtandao wa Eyewitness news uliopo Afrika Kusini amesema “Moja ya mambo muhimu tunayofanya ni mzunguko wa wachezaji. Kikosi chetu cha wachezaji 28 kwa kiasi kikubwa wote wana kiwango sawa kwa hivyo hiyo imetusaidia sana msimu huu. Benchi la ufundi limeweza hilo vizuri sana. Nataka kuwapongeza kwa jinsi wanavyocheza katika Kombe la Shirikisho Afrika.”

Baadhi ya wachezaji wa Yanga wakiwa na kocha wa viungo.

Hersi Said pia amezungumzia historia ya Yanga katika nchi lakini pia kwa kiasi gani ambavyo ilipata tabu baada ya kuachana na aliekua mfadhili wao Yusuph Manji.

Rais huyo pia hakusita kuelezea uwekezaji waliouweka na nguvu ya Wanachama wa Yanga na kusema mafanikio hayo yalitafutwa hayakuja tuu kutokea popote.

“Ni klabu kongwe zaidi nchini na imekuwa ikienda tangu 1935. Ilikuwa ni sehemu ya jamii iliyopigania uhuru. Tulikuwa na mfadhili miaka michache iliyopita ambaye alihama na kuondoka nchini na klabu iliyumba kutokea hapo. Hatukuweza kulipa mishahara na tuliporomoka katika suala la mafanikio na kupataka matokeo mabaya mwaka 2016/17,” alisema na kuongeza,” alisema na kuongeza

Viongozi wa Yanga na GSM katika hafla ya utiaji saini ya uhusiano na Laliga.

“Kampuni yangu iliamua kuja na kufadhili klabu na tukaja na mabadiliko kwa klabu. Tulishirikiana na La Liga na kushauriwa kuhusu njia ya kisasa ya kuendesha klabu na wanachama na mashabiki walipigia kura mabadiliko. Tuna wanachama 70,000 waliosajiliwa ambao wanalipa ada zao ambazo husaidia uendeshaji wa klabu kwa kiasi kikubwa.

Hatuna wachezaji ambao tulikuwa nao miaka 3 iliyopita, mimi ndiye nimesajili wachezaji wote wapya na kujenga timu kutoka mwanzo. Sio kitu ambacho kilitoka bila kupangiliwa.”

Sambaza....