Chama Cha Soka mkoa wa Pwani COREFA Agosti 27 kitafanya uzinduzi wa kituo cha pili cha michezo wilayani Mkuranga mkoani Pwani ikiwa ni muendelezo wa mikakati ya Mwenyekiti Robert Munisi wakuhakikisha kwamba kila Wilaya inakuwa na vituo hivyo.
Kituo hicho cha pili kitazinduliwa katika shule ya msingi Mkuranga kuanzia saa tano asubuhi na kuhudhuriwa na wageni mbalimbali ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya Mhe. Hadija Nasiri Ally.
COREFA inakwenda kuzindua kituo hicho cha pili ambapo kituo cha kwanza kilizinduliwa Agosti 20 na Katibu Tawala Mosses Magogwa ,katika uwanja wa Bwawani Kibaha Mkoani Pwani ambapo jumla ya vijana zaidi ya miasita 600 wenye umri wa miaka 15, 17 na 20 walisajiliwa katika kituo hicho.
“Tunakwenda kuweka rekodi nyingine ndani ya Wilaya ya Mkuranga, lengo ni kuhakikisha kwamba mpira mkoa wa pwani unachezwa,” alisema Christina Mwagala afisa habari wa Corefa na kuongeza;
“Kituo hiki kitakuwa na manufaa kwa vijana wanaopenda mpira kutimiza ndoto zao, ni zamu ya watu wa Mkuranga sasa kunufaika na COREFA ambayo inataka kufanya mambo makubwa katika mpira wetu ndani ya mkoa wa Pwani.”
“Aidha jambo hili nikubwa na niheshima kwa watu wa Mkuranga hivyo nitoe wito siku ya Jumapili kujitokeza kwa wingi kwa lengo la kufanikisha uzinduzi huo wa kituo cha michezo kwa vijana wetu kwani wote tunafahamu kuwa mpira ni ajira,” alimalizia Mwagala.