Sambaza....

Misimu miwili iliyopita Sadio Kanoute “Putin” alikuwa anatoa ubora wa hali ya juu sana kwenye eneo la kiungo la Simba SC lakini msimu huu hajaanza vizuri sana kwenye mashindano kama ambavyo ilikuwa miaka miwili nyuma.

Mechi za mwanzo dakika alizocheza ameonekana kukosa wakati mzuri sana kwenye eneo lake, hiyo imefanya sasa anaanzia nje na Fabrice Ngoma ndio chaguo la kocha kwenye eneo alilokuwa anacheza Sadio Kanoute “Putin”.

 

Nguvu yake, utulivu na kujiamini ndani ya uwanja ni kama imepotea kabisa mbaya zaidi ni wakati ambao timu inamhitaji sababu Fabrice Ngoma naye bado anahitaji dakika nyingi zaidi ili kutoa huduma nzuri katika eneo la kiungo la Simba.

Benchi la ufundi wanatakiwa kuhakikisha Sadio Kanoute anarudi kwenye ubora wake ili Simba iwe salama zaidi katika eneo hilo. Je, umeishawaza itakuwaje pale ambapo Ngoma au Mzamiru mmoja akiumia kwa bahati mbaya na akahitajika kuwa kwa muda mrefu?

Fabrice Ngoma.

Hii itakuwa hatari kubwa sana ndani ya timu kwa kuzingatia mchezaji ambaye anaweza kuwa mbadala wa hao bado hayupo kwenye kiwango bora. Sadio Kanoute anahitaji kuongeza juhudi kwenye uwanja wa mazoezi ili apate dakika nyingi uwanjani kama ilivyokuwa miaka miwili nyuma.

Rahisi! Kama umeangalia kwa umakini mkubwa mechi za Simba za hivi karibuni utakuwa umeona shida katika eneo la kiungo! Mzamiru Yassin naona anaiokoa sana timu katika eneo la kiungo sababu Fabrice Ngoma naye bado anahitaji mechi za ushindani zaidi ili kuwa imara.

Mzamiru Yassin.

Kitu hatari kwao wanapitia shida hiyo kwenye eneo la kiungo ikiwa ni wakati ambao wanamkosa pia mlinzi wao wa kati Henock Inonga ambaye mara kadhaa amekuwa akificha makosa ya timu ambayo huanzia eneo la kiungo.

Binafsi naona Mzamiru Yassin anapitia wakati mgumu sana kwenye eneo la kiungo sababu hana msaada kutoka kwa Sadio Kanoute na Fabrice Ngoma ambao hawapo vizuri kwa sasa na wanahitaji subira ili kutoa ubora wao kwa asilimia 100.

Sambaza....