Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika ‘CAF’ limeweka wazi majina ya waamuzi watakaocheza mechi mbili za kuwania Kufuzu kwenye michuano ya mataifa Afrika mwakani kati ya Cape Verde na Tanzania.
Majina ya waamuzi hao yanahusisha mechi ya kwanza Itakayofanyika nchini Cape Verde kwenye uwanja wa Estádio Nacional de Cabo Verde, mjini Praia Septemba 12, pamoja na ule wa marudiano utakaofanyika jijini Dar es Salaam Septemba 16 mwaka huu.
Kwenye mchezo utakaofanyika nchini Cape Verde, Mwamuzi wa kati atakua Boubou Traore akisaidiwa na Mwamuzi namba moja Drissa Kamory Niabe, Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Baba Yomboliba na Mwamuzi wa akiba Gaoussou Kane wote wakitokea nchini Mali na Kamishna wa Mchezo anatokea Gini ya Ikweta ambaye ni Tadeo Nsue Onva.
Aidha mchezo wa marudiano kwa timu hizo utakaochezwa Oktoba 16, 2018 Kwenye Uwanja wa Taifa wenyewe utachezeshwa na Waamuzi kutoka Djibouti, ambapo Mwamuzi wa kati atakuwa Souleiman Ahmed Djama, na Mwamuzi msaidizi namba moja ni Farhan Bogoreh Salime, Mwamuzi msaidizi namba 2 Rachid Waiss Bouraleh na Mwamuzi wa akiba Bilal Abdallah Ismael.
Kamishna wa mchezo anatokea nchini Malawi Maxwell Mtonga, Mtathmini waamuzi anatokea Rwanda na atakuwa ni Michael Gasingwa.
Ikumbukwe Katika msimamo wa Kundi L, timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inashika nafasi ya tatu wakiwa na alama mbili, ili hali Uganda ndio wanaoongoza kwa alama 4 wakifuatiwa na Lesotho wenye alama mbili na Cape Verde wanashika mkia wakiwa na alama Moja.