Kiungo mshambuliaji raia wa Ghana Augustine Okrah amepona majeraha yake yaliyomuweka nje kwa muda mrefu na sasa yupo tayari kuwatumikia Wekundu wa Msimbazi Simba wakati hali ikiwa mbaya kwa mlinzi wa pembeni Shomary Kapombe.
Mara ya mwisho kwa Okra kuonekana uwanjani ni miezi miwili iliyopita katika mchezo wa kirafiki kati ya Simba Sc na Al Hilal ambapo aliumia kipindi cha pili na kulazimika kutolewa nje ya uwanja na kushindwa kuendelea na mchezo.
Kupitia taarifa rasmi ya klabu Simba wamethibitisha urejeo wa Mghana huyo ambae katika mchezo wa raundi ya kwanza dhidi ya Yanga alifunga bao katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja.
Nae mlinzi wa pembeni wa Simba Shomary Kapombe aliepata majeraha katika mchezo dhidi ya Raja Casablanca na kutolewa katika dakika za mwishoni atakaa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja.
Majeruhi hayo sasa yatamfanya Kapombe kukosa michezi miwili ya timu yake dhidi ya Ihefu na mchezo wa Watani wa Jadi Aprili 16 mwaka huu. Ni wazi sasa pengo lake litazibwa na Israel Mwenda aliepona majeraha yake na kurudi kikosini.
Ndani ya mwezi huu April Simba itakua na michezo mingine miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali na mpinzani wao watamjue leo jioni kwenye droo itakayofanyika nchini Misri saa tatu usiku.